Ufunuo 14:13 “Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao”

Katibu Mkuu wa KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mwl. Julius Madiga kwa niaba ya Uongozi wa KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki anasikitika kutangaza kifo cha Mwj. Ridas Edward Jani kilichotokea usiku wa kuamkia  tarehe 17/12/2023 nyumbani kwa marehemu Majengo Juu Hale.

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewashukuru na kuwapongeza wanadayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa kujitoa kikamilifu katika kuchangia fedha kwaajili ya kulipa deni la Dayosisi, ambapo amewasihi kuongeza jitihada katika kuchangia deni hilo ili liweze kuisha na Dayosisi  kuendelea kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.

 

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ametoa  salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,Watanzania wote pamoja  na ndugu waliopoteza wapendwa wao, kufuatia maafa ya mafuriko, yaliyosababishwa na  mmomonyoko wa ardhi kufuatia kumeguka kwa sehemu ya Mlima Hanang uliopo Mkoani Manyara ambao ulikuwa na miamba dhoofu iliyonyonya maji na kusababisha maporomoko na hivyo kutengeneza tope ambapo pamoja na mvua kubwa iliyokuwa inanyesha tope hilo lilisambaa katika makazi ya watu na kusababisha maafa makubwa.

Askofu Dkt. Mbilu ametoa salamu  hizo tarehe 10/12/2023 kwenye Ibada ya Jumapili ambayo inafunga kalenda ya matukio ya Dayosisi iliyofanyika Kanisa Kuu Lushoto na kusisitiza kuwa Kanisa linaungana na Wananchi waliokumbwa na maafa hayo ya mafuriko na hivyo kuagiza Jumapili ya Tarehe 17/12/2023 kuwepo na maombi maalumu yatakayo ambatana na toleo maalumu (SADAKA) itakayo tolewa katika Sharika zote za KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, na  ili kiasi cha pesa zitakazo patikani zitakabithiwa kwa uongozi wa Serikali kama sehemu ya Mkono wa pole kufuatia maafa hayo. 

MBUNGE WA LUSHOTO MHE. SHABANI SHEKILINDI

Naye Mbunge wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Shekilindi ameunga mkono jitihada za Askofu Dkt. Mbilu katika kuhakikisha deni lote la Dayosisi linamalizika kwa kuchangia kiasi cha Shilingi Milioni Moja na Laki Mbili na Elfu Kumi(1,210,000/=) na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Kanisa.

Ibada hii ilihudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Dayosisi akiwemo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Bi. Ikupa Harsoni Mwasyoge, ambaye katika salamu zake ameishukuru KKKT-DKMs, kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo mbalimbali ikiwemo utunzaji wa mazingira.

Hata hivyo Mhe. Ikupa Mwasyogenaye, amemshukuru kipekee, Askofu Dkt. Mbilu kwa kuagiza sharika za KKKT-DKMs, kufanya changizo maalumu la kutoa sadaka na vitu mbalimbali Jumapili ya tarehe 17/12/2023 kwaajili ya kuwasaidia waathirika wa mafuriko Mkoani Manyara kwani kwa kufanya hivyo ni sehemu ya kuunga mkono wito alioutoa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya kuwasaidia waathirika hao.

 

DEAN MICHAEL MLONDAKWELI KANJU

Katika Ibada  hii jumla ya vijana 71 walibarikiwa na wa 5 kubatizwa ambapo kwenye risala yao waliyoisoma kwa Baba Askofu Dkt. Mbilu, wamesema kuwa wanatambua kazi kubwa inayofanywa na KKKT-DKMs katika kumhudumia mwanadamu kiroho, kimwili na kiakili na hasa kazi za maendeleo zinazoendelea kufanyika, huku wakiahidi kwenda kuwa vijana wenye nidhamu na watii katika Kanisa na jamii kwa ujumla.

Vijana wa kipaimara walitoa kiasi cha Tsh 250,000 kwaajili ya kuchangia ulipaji wa deni la Dayosisi, ambapo pia waliomba kuungwa mkono na wazazi,walezi pamoja na washarika walioshiriki katika Ibada na kufanikiwa kukusanya jumla ya Ths. 3,448,550/= ambapo fedha hizo zimeelekezwa katika kulipa deni la Dayosisi.

MKUU WA JIMBO LA KUSINI. MCH. ISSAI AMASIA MWETA

 

 Sisi Wachungaji na Mashemasi wastaafu, watumishi tulioitumikia KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu Mwenyezi kwa jinsi anavyoendelea kututunza na kutubariki katika maisha yetu.Tunaamini kwamba katika historia imekuwa jambo la kipekee kuweza kukutana na kukaa kwa faragha pamoja na uongozi mzima wa Dayosisi yetu. Kwa hakika imekuwa nafasi muhimu lakini adhimu.

Tunayo kumbukumbu kwamba uongozi uliopo madarakani kwa sasa uliingia madarakani kuiongoza Dayosisi yetu katika kipindi kigumu sana, hasa tukizingatia mambo kadhaa ya msingi:

1.Ni kipindi ambacho Dayosisi ilikuwa imegawanyika sana

2.Waumini wa Dayosisi hii, walikuwa katika hali ya kukata tamaa kiasi cha baadhi yao kuwa wameihama Dayosisi yetu.

3.Sharika zetu na Dayosisi yetu kuonekana kutokuwa na mwelekeo thabiti.

4.Wachungaji, Mashemasi na waumini kugawanyika na hivyo kutoaminiana.

Hali hii imeufanya uongozi mpya wa Dayosisi uliopo madarakani kuwa na kazi ngumu ya mahali pa kuanzia, ingawa tunamshukuru Mungu kwa Neema yake kwa kuupa uongozi mpya Neema ya kuyaona hayo na kuamua kuanza kuchukua hatua nzuri na madhubuti kuiweka Dayosisi yetu katika mstari kwa kutengeneza na kujenga mwelekeo mpya.  Miongoni mwa mambo muhimu tuliyoona yakifanyika ni pamoja na:

  1. Kurudisha mioyo ya waumini waliokata tamaa na mambo ya kiimani

2.Kuona namna ya kurudisha kwa upya uhusiano katika kuaminiwa na Serikali na marafiki zetu.

3.Uongozi wa kujiamini na kujenga moyo wa utayari katika kujitoa kutumika na sio kutumikiwa.

Tumeshuhudia kwa wazi jinsi mwelekeo huo mpya ulivyowekwa wazi katika kutumika kwa nguvu zote na kujenga upya Imani ya waumini na marafiki. Miongoni mwa mambo tuliyoshuhudia ni pamoja na:

  1. Uendelezaji wa miradi ikiwa ni kwa ajili ya kuifanya Dayosisi ilenge kujitegemea katika kipindi kijacho. Tunaona miradi ya vibanda vya biashara, kilimo, na kadhalika.

Kazi hizi zinazofanyika na nyingine nyingi zinazotazamiwa zinachagiza mchango mkubwa kwa maendeleo ya haraka ya Dayosisi yetu kurudi katika mstari kwa upya.  Imani yetu ni kwamba, mambo haya yatairudisha Dayosisi yetu mahali pake.

Kwa ajili hiyo sisi Wachungaji na Mashemasi wastaafu, tuliokutana hapa KOTETI tarehe 28 hadi 29 Novemba, katika mwaka wa Bwana wetu, tunatumia nafasi hii kuupongeza uongozi Mpya wa Dayosisi yetu, kwa kipekee kinara mapambano ambaye ni Mheshimiwa Baba Askofu Dr. Msafiri Joseph Mbilu.  Sisi Wachungaji na Mashemasi Wastaafu tunaweka ahadi kwake kwamba tutaendelea kumwombea afya njema na kumsaidia. Aidha tunamwambia kwamba kustaafu sio kuacha utumishi ila kustaafu ni kuwa uwanja mpya wa mapambano ya kiutumishi.

            Ni sisi Wachungaji na Mashemasi wastaafu

            Tumeitoa leo tarehe 29 Novemba, 2023.