Print

Wapendwa  wana KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki yahusu ziara rasmi ya kikazi ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Baba Askofu Dkt. Fredrick O. Shoo katika Dayosisi yetu kuanzia tarehe 27/07/2022 hadi tarehe 02/08/2022.

 Dhumuni la ziara ya Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo ni kuitembelea KKKT – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, kufungua na kuweka mawe ya msingi. Vilevile Baba Askofu Dkt. Shoo atapata wasaa wa kuongea na wana Dayosisi katika maeneo mbalimbali.

 Baba Askofu atawasili katika Dayosisi yetu tarehe 27/07/2022 siku ya jumatano saa 4:00 asubuhi, punde atakapokanyaga ardhi ya Mkoa wa Tanga katika eneo la Bwiko atapokelewa na mwenyeji wake Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu na wana Dayosisi. Ataanza ziara yake siku hiyohiyo ya tarehe 27/07/2022 katika Jimbo la Tambarare kwa kuweka jiwe la msingi la Kanisa jipya katika Usharika wa Mombo muda saa 6:00 mchana.

 Aidha mara baada ya uwekwaji wa jiwe la msingi msafara wa Mkuu wa KKKT utaelekea katika Jimbo la Kusini ambapo Baba Askofu Dkt. Shoo ataongea na wana Dayosisi katika Usharika wa Soni yalipo Makao Makuu ya Jimbo hilo majira ya saa 10:00 jioni. Mara baada ya kuongea na wanadayosisi katika Usharika wa Soni siku hiyohiyo msafara utaelekea Kanisa Kuu Lushoto ambapo Mkuu wa KKKT atapokelewa rasmi kwa Ibada maalum saa 11:45 jioni.

 Tarehe 28/07/2022 msafara wa Mkuu wa KKKT utaelekea Bumbuli kuanzia saa 2:00 – 6:00 mchana, ambapo Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo ataendelea na ziara yake katika Jimbo la Kusini kwa kutembelea Usharika wa Bumbuli, Hospitali ya Bumbuli na Chuo cha Utabibu Bumbuli (BUCOHAs).

Majira ya saa 7:30 mchana hadi saa 12:00 jioni msafara wa Mkuu wa KKKT utaelekea Lutindi ambapo Baba Askofu atapata wasaa wa kuwasalimu washarika wa Lutindi na kutembelea Hospitali ya wagonjwa wa akili Lutindi (Lutindi Mental Hospital).

 Siku ya tarehe 29/07/2022 msafara wa Mkuu wa KKKT muda wa saa 3:00 hadi 6:00 mchana  utaelekea katika Jimbo la Tambarare ambapo itafanyika Ibada katika Usharika wa Korogwe na majira ya saa 7:00 mchana msafara utaelekea Jimbo la Pwani.

 Tarehe 30/07/2022 saa 3:00 – 6:00 mchana Baba Askofu ataweka jiwe la Msingi wa Kanisa la Makorora na kuongoza Ibada ya kipaimara katika Usharika huo wa Makorora.

 Tarehe 31/07/2022 Mkuu wa Kanisa ataongoza Ibada ya jumapili Kanisa Kuu Lushoto kuanzia saa 2:00 – 5:00 asubuhi na majira ya saa 8:00 – 10:00 jioni atatembelea vituo vya Irente Rainbow School, Irente Children’s Home, Irente School for the Blind na Irente Farm.

 Tarehe 01/08/2022 saa 4:00 – 5:00 asubuhi msafara wa Mkuu wa Kanisa utaelekea katika Jimbo la Kaskazini ambapo pia kutafanyika Ibada katika Usharika wa Mlalo na majira ya saa 6:30 -8:00 mchana ataelekea katika Shule ya Sekondari Lwandai ambapo Baba Askofu Dkt. Shoo atafungua tena Jengo la Maabara ambalo lilifanyiwa ukarabati  na majira ya saa 9:00 – 11:00 jioni msafara wa Mkuu wa Kanisa utaelekea katika Chuo  kitarajiwa cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI).

 Wito kutoka kwa Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kwa wana KKKT – DKMs, ni kujitokeza kwa wingi kumpokea Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo sehemu zote atakazopita kuanzia Bwiko, Soni, Lushoto, Mlalo, Bumbuli, Lutindi, Tanga, Korogwe na maeneo yote yaliyotajwa atakapokuwa anatembelea, anafungua, anaweka mawe ya msingi na atakapokuwa anaongea nasi.

 Mwisho kama ilivyo kawaida na desturi ya wana KKKT-DKMs wakati tunapotembelewa na wageni hasa ugeni mkubwa wa Mkuu wetu wa KKKT, Baba Askofu Dkt. Fredrick O. Shoo, natoa wito tena kwenu kujitokeza kwa wingi tumpokee Mkuu wetu wa Kanisa katika Dayosisi yetu.