
Viongozi mbalimbali wa serikali, dini pamoja na wataalam wa Elimu ya watu maalum wenye ulemavu wametakiwa kusimamia na kuhimiza haki na usawa wa kielimu kwa kushirikiana na jamii ili kuondoa dhana potofu katika jamii kuwa watu wenye ulemavu hawana uwezo wa kufanya jambo lolote katika jamii kwasababu ya hali waliyonayo.
Wito huo umetolewa na Msaidizi wa Askofu Mteule wa KKKT DKMs Mch. Frank Mntangi wakati alipokua akitoa hotuba yake katika ufunguzi wa warsha ya Elimu maalum yenye dhamira kuu ya "Elimu maalum kwa mafanikio ya baadae" inayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Elimu ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) iliyopo katika Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga.
Amesema wapo watoto wenye ulemavu ambao wanauwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo katika familia, jamii na Taifa kwa ujumla lakini bila mfumo jumuishi wa elimu unaotambua na kuheshimu mahitaji yao maalumu ipo hali ya kupoteza vipaji hivyo na kuua ndoto zao.
Dean Mteule Mntangi amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetengeneza Sera na Sheria mbalimbali zinazo watambua na kuwalinda walemavu ambazo zina ainisha na kutambua ujumuishaji na upatikanaji wa huduma za kijamii kwa watu wenye ulemavu hivyo ni vema Viongozi wakashirikiana katika kuhakikisha jamii inawatambua na kuwathamini ikiwa ni pamoja na kupata haki sawa ikiwemo haki ya kupata elimu.
Kwa upande wao washiriki wa warsha hiyo wamesema kuwa kupitia warsha hiyo watapata nafasi ya kujadili mambo mengi kuhusu elimu jumuishi huku wakitoa wito kwa jamii kuamka na kuhakikisha walemavu waliopo katika jamii wanapata haki zao za msingi.
Warsha hii ni ya siku tatu ambayo imeanza leo tarehe 12/06/2025 na itahitimishwa tarehe 14/06/2025 na imeandaliwa na KKKT-DKMs chini ya Kurugenzi ya huduma za jamii kwa kushirikiana na Dayosisi rafiki ya Lund Sweden.
Warsha hii imewakutanisha wadau kutoka Mikoa mbalimbali, Taasisi binafsi na za serikali ikilenga kufikia lengo la kuweka msingi imara katika kuhakikisha Taasisi ya KOTETI inatoa Elimu maalumu kama ilivyokuwa SEKOMU.







