Print

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt Msafiri Joseph Mbilu ameongoza Ibada ya kuingizwa  kazini  kwa Katibu Mkuu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Godfrey Tahona Walalaze, Mkurugenzi wa fedha na utawala CPA Peter John Singano pamoja na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya KKKT-DKMs, leo tarehe 06/02/2022 katika Usharika wa Korogwe.Katika kikao cha Halmashauri Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki  iliyoketi Utondolo Lushoto tarehe 9-10/12/2021 ilimthibitisha Mch. Godfrey Walalaze Kuwa Katibu Mkuu na CPA Peter John Singano kuwa Mkurugenzi wa fedha na Utawala.

 


Sehemu ya Itikio na Shukurani kwa Kuingizwa katika wajibu wa Katibu Mkuu- KKKT-DKMs Mch.Godfrey Tahona Walalaze

Mhashamu Askofu, Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu,Mpendwa Baba Askofu Mstaafu Mch. Joseph Mathayo Jali Mhe. Mhandisi Robert Kitundi- Katibu Mkuu KKKT-DKMs Mhe. Dean Mch. Michael Mlondakweli Kanju -Dean KKKT-DKMs Mhe. Mch. Adv. Elias Mollel Katibu Mkuu KKKT-Magharibi Kati (Tabora) Mhe. Mathias Msemo Katibu Mkuu KKKT- Dayosisi ya Mwanga,Mhe. John Tanaki, Katibu Mkuu KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Kati (Arusha) Mhe. Mch. Issay Mweta- Mkuu wa Jimbo la Kusini,Mhe. Mch. Anderson Kipande- MKuu wa Jimbo la Kaskazini,Mhe. Mch. Frank Mntani- Mkuu wa Jimbo la Tambarare,Mhe. Mch. Thadeos Ketto- Mkuu wa JImbo la Pwani,Waheshimiwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya KKKT- DKMs,Mhe. Peter John Singano Mkurugenzi wa Fedha na Utawala,Mhe. Mch. Dtk. William Kopwe -K/Mkurugenzi HZJ,Mhe. Bw. Davidi Chanyeghea  K/Mkurugenzi Uchumi, Mipango na Maendeleo,Wapendwa Wachungaji wenzangu,Wakuu wa Idara mbalimbali za DKMs,Wapendwa Mashemasi
Wapendwa Wainjilisti,Wapendwa Wenzi wa Wachungaji,Wapendwa Wazee wa Kanisa,Watumishi wa Ofisi Kuu- DKMs,Wapendwa Familia ya Walalaze, Singano,Wapendwa Wageni toka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Dayosisi,Wapendwa Wakristo Wenzangu, Mabibi na Mabwana,Bwana Yesu Kristo Asifiwe.



“Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi?Msaada wangu u katika BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi. Asiuache mguu,wako usogezwe, Asisinzie akulindaye; Naam, hatasinzia wala hatalala,usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israel. Bwana ndiye mlinzi wako, BWANA ni uvuli mkono wako wa kuume. Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku. Bwana atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.” Zab 121:1-8. Awali ya yote ninamshukuru Mungu ambaye kwa rehema na neema yake amenijalia kufikia siku hii na kunipa Kibali cha kusimama mbele yake na mbele yako wewe Mha Askofu na watumishi wenzangu kwa kuupokea wito na wajibu huu wa Katibu Mkuu wa KKKT - Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.



Ninakiri kuwa sina uwezo utoshao ila ni huruma yake Kristo inayonipa kibali na nguvu za kuendelea kutumika ndani ya Dayosisi yetu na katika nafasi hii nyeti na muhimu kwa Dayosisi yetu katika kipindi kilicho na changamoto kubwa na za kipekee za wingi wa madeni tuliyoyarithi. Kwa kipindi kifupi cha mwaka mmoja ambao nimetumika ndani ya ofisi hii, kimenipa picha ya uhalisia na ugumu wa ofisi hii. Kama ingekuwa ni kuomba ingenitafakarisha mara mbili, lakini kwangu ninaupokea wajibu huu kama wito, wito ambao ndio kiapo changu cha msingi mbele za Mungu kwa
huduma ya Uchungaji, wito wa kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa. Nikikumbushwa kila mara na Yoh 15:16 Kristo anaposema na wanafunzi wake kuwa “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi, nami nikawaweka mwende mkazae matunda, na matunda yetu yapate kukaa; ili kwamba lolote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.” Kwa kutambua na kuthamini kusudi la Mungu kwa kila majira, na kuzingatia kuwa yeye ndiye anayetuita kwa kila wajibu ndani ya Kanisa lake,  ninapenda leo hii kukuhakikishia, Baba Askofu, kuwa nimeupokea wito huu na niko tayari kuungana nawe kama msaidizi wako wa karibu katika kutimiza majukumu unayopaswa kuyatimiza ili kuiinua Dayosisi na Kanisa kwa ujumla.

Nitatazamia mara zote uongozi na hekima yako katika kuniwezesha kuwa msaidizi mwenye tija kwa utumishi wako na ustawi wa Dayosisi, Kanisa na taifa letu kwa ujumla. Ninakuahidi mbele za Mungu Mtakatifu kuwa, kwa unyenyekevu na uthabiti nitakupa ushirikiano mpevu, utakaozingatia haki, ukweli na uaminifu ili kuifikia Kasi tofauti yenye kuzingatia viwango, Umakini, Uadilifu na Uharaka katika kufanya maamuzi na kuyasimamia.
Kwa unyenyekevu nitakushauri na kwa ujasiri nitatekeleza maamuzi yote yatakayoimarisha Umoja na Mshikamano kwa kuongozwa na taratibu, miongozo, kanuni na sheria kama zilivyo katika Katiba ya Dayosisi, na itakavyoamuliwa mara kwa mara katika vikao mbalimbali vya Dayosis; Nitayafanya hayo nikizingatia kuyatafsiri na kuyatekeleza maono yako na kwa pamoja tuweze kufikia viwango Mungu alivyoikusudia Dayosis yetu na hivyo kuujenga mwili wa Kristo usio na mawaa. Nitakuwa tayari kwa umakini na hekima kuwa muwakilishi mbele ya jamii na Serikali pale utakaponituma kufanya hivyo nikizingatia kuyaendeleza mahusiano yetu mazuri na serikali, jamii na taasisi mbalimbali zinazotumika pamoja nasi.

SHUKRANI:
Ninapenda Kumshukuru Mkuu wa Kanisa na kipekee Katibu Mkuu wa KKKT, Mhandisi . Robert Kitundu kwa ushirikiano mpevu wa kirafiki katika kuianza huduma hii, ninakuahidi kuwa kama mmoja wa wajumbe wa HKUU ya Kanisa nitakuwa kiungo muhimu kulitimiza kusudi la Mungu kwa Kanisa lake. Ninapenda kuishukuru Halmashauri Kuu ya KKKT-DKMs kwa kuamini kuwa toka katika chombo hiki dhaifu linaweza tokeza jambo la kutumainiwa. Kwa msaada wa Mungu sitawaangusha ninyi na Wakristo wote wa KKKT-DKMs, Ninawashukuru Makatibu Wakuu wenzangu ambao wamejitoa kipekee kuifanya siku hii iwe na sura ya kipekee. Mungu azidi kutupa ushirikiano na kudumu katika kulitumikia Kanisa lake ulimwenguni mwote, Ninapenda kuwashukuru familia yangu ndogo ya Youth Peacemakers, mmekuwa mtango jangwani kwa muda mrefu na kuwa sababu ya kusonga mbele pasipo mashaka juu ya uwezo wa Mungu kwa watu wanaomtegemea. Mungu azidi
kuwainua.

Ninapenda kwa upekee sana kumshukuru Mke wangu , watoto wangu na familia yangu ambayo wakati wote imesimama nami katika wajibu na wito wangu, iliponyesha mvua walitoa miamvuli nisilowe, lilipowaka jua kali waliweka nyasi juu yangu nisije nikajuta. Kwenu ninyi nisema Bwana hakuwaita kwa bahati mbaya, aliwakusudia kuwa sehemu ya wito huu, naye atawalipa kwa
kadri ya wingi wa Fadhili zake.

Mwishoni pasipo kuwachosha sana, niwashukuru ninyi nyote ambao kila mmoja amekuwa sehemu ya safari hii hata kufikia siku hii. Mha Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, niseme tena kwa uthabiti,
Ninaipokea nafasi hii kwa unyenyekevu mkubwa, na niko tayari kutumika pamoja nawe.  “Nitayainua macho yangu niitazame milima, msaada wangu utatoka wapi, msaada wangu u katika Bwana aliyezifanya mbingu na Nchi.”

Sehemu ya itikio na Shukurani kwa Kuingizwa katika wajibu wa kuwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawa- KKKT-DKMs CPA Peter John Singano.

 

Mhe. Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu Mkuu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Katibu Mkuu KKKT Eng. Robert Kitundu, Mhe. Dean Mch. Michael Mlondakweli Kanju, Katibu Mkuu Mch. Godfrey Walalaze, Makatibu wakuu wa Dayosisi za KKKT, wajumbe wa Halmashauri Kuu, wakuu wa majimbo, wachungaji wote,watumishi wenzangu Ofisi kuu ya KKKT-DKMs, washarika wote, wageni waalikwa mabibi na mabwana Bwana wetu yesu Kristo asifiwe!

Nichukue nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kunipa wajibu huu wa kutumika kama Mkurugenzi wa Fedha na Utawala KKKT-DKMs, nimshukuru Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu mshika maono wa Dayosisi yetu kwa kuniamini kuwa sehemu ya watendaji wake kuanzia mwezi wa sita mwaka 2021 nilivyoanza kukaimu nafasi hii hadi pale Halmashauri Kuu ilivyonithibitisha kwenye kikao kilichofanyika tarehe 9-10/12/2021 Utondolo Lushoto

 

Nina washukuru wajumbe wa Halmashauri Kuu kwa kuniamini na kunithibitisha.Imani hii inanipa nguvu ya kutumika na kujitahidi katika utumishi wangu. Baba Askofu nimepokea wajibu huu kwa moyo wote, kwa ajili ya kukusaidia katika maono uliyobeba kwa ajili ya Dayosisi yetu. Mungu akubariki sana.

Ninapenda kumshukuru kipekee Baba Dean Mch Michael Mlondakweli Kanju kwa maelekezo yake mbalimbali, nimshukuru pia Katibu Mkuu  Mch. Godfrey Walalaze kwa miongozo yake, ushauri wake kama mtendaji mkuu wa Dayosisi yetu. Ninawashukuru Wakuu wa Majimbo,mwenyekiti wa halmashauri ya Mipango na Fedha, Dr. Stephen Magesa, kwa jinsi tunavyoshirikiana, wachungaji wote, watumishi wenzangu wa Ofisi Kuu, vituoni na sharikani. Pia ninamshukuru sana Mama yangu mzazi Catherine Singano mke  wangu kijana wetu Adriel Peter Singano, ndugu jamaa na marafiki wote. Mungu awabariki sana.

 

Ninawaomba sana mniombee, mnishauri katika kutimiza wajibu wangu kama ilivyoelekezwa katika Katiba yetu ya KKKT-DKMs. Tunazo changamoto nyingi ikiwemo ya madeni mengi, kufufua vituo vyetu. Hivyo niwaombe wakristo na washarika wenzangu kushirikiana na kuombeana.

Mwisho niushukuru uongozi wa KKKT-DKMs kwa kutoa wazo la kuwa na  sadaka ya maendeleo ninaomba tuingie kazini ili sadaka hii iweze kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye Dayosisi yetu pia kuimarisha na kuleta maendeleo ya Dayosisi yetu.

“Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, sisi tu watumwa wasio na faida, tumefanya tu yaliyopasa kufanya” Luka.17:10

Baada ya kesema hayo napenda kusema kuwa nimepokea wajibu huu kutumika shambani mwa Bwana na Mungu anisaidie.