Print

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewapa maagizo wakuu wa majimbo kusimamia shughuli nzima ya zoezi la kuhakikisha kila kijana anachangia bati moja katika ujenzi wa shule ya Bangala Lutheran Junior Seminary pia amewataka vijana watumie tamasha hilo kuunganisha mahusiano yao kwa kunyanyuana kiuchumi sambamba na kurudi kwa Mungu.

Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo leo Jumapili ya tarehe 27/02/2022  katika Ibada ya tamasha la Askofu na vijana lililofanyika katika ukumbi wa Benjamin Mkapa SEKOMU ambapo zaidi ya vijana wapatao 1500 wameshiriki katika tamasha hilo.

akihubiri neno la Mungu kutoka  kitabu cha ISAYA 35 3-5 “Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu yafanyeni imara magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, jipeni moyo, msiogope, tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu, atakuja na kuwakoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa na masikio ya viziwi yatazibuliwa”

Naye Askofu mstaafu wa KKKT-DKMs mzee Joseph Jali amewahimiza vijana kujitoa  kufanya kazi ya Mungu na amefurahishwa kwa jinsi vijana walivyoshiriki tamasha hilo kwa wingi “Macho yangu yameona vijana wengi kama maua imenipa nguvu na kuamini kuwa  KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki nguvu ya Utume wa Mungu ipo”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa vijana KKKT Bw. Julian Kagambo amesema kuwa Halmashauri kuu ya vijana  iko pamoja na uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na walikua wanaugua sana kwa sababu ya kutokushiriki kwa muda mrefu, lakini kwa sasa vijana wa KKKTs-DKMs wamepata Askofu ambaye ameonyesha unyenyekevu mkubwa kwa vijana.

Kwa msisitizo ameongezea kuwa mwenyekiti wa vijana wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki aite viongozi wakafanyie kazi jukumu walilopewa na baba Askofu la kila kijana kuchangia bati moja kwa ajili ya maendeleo ya shule ya Bangala Lutheran Junior Seminary na kuacha alama katika Dayosisi.

Vijana wana hazina kubwa sana lakini wana uchoyo kwa hiyo ni muda sasa wa kujitoa na kuacha alama katika Kanisa kwa kujishughulisha katika maendeleo ya Kanisa wawe na maono na kuacha ubinafsi na kusimama katika majukumu yao.