Print

 

Uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kupitia kwa Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu umeanza utekelezaji wa ahadi waliyoitoa juu ya utaoji wa taarifa  ya  fedha zinazochangwa na Wanadayosisi zitakazo saidia kukabiliana na Deni la Dayosisi.

Ikumbukwe kua mnamo tarehe 24/03/2022 Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu aliwaandikia barua wana Dayosisi kuwaomba kuingia kazini ili kukabiliana na madeni makubwa yanayoikabili Dayosisi ambayo kwa ujumla wake ni hatarishi kwani yanaweza kusababisha mali za Dayosisi kupigwa mnada, kudumaza Dayosisi kwa muda mrefu, kutokuaminiwa na wadau wa maendeleo, kuathirika kwa Misioni pamoja na kufisha maono ya viongozi.

Na hii ni sehemu ya barua ya shukrani ya Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu iliyosomwa leo tarehe 01/05/2022 katika Sharika za KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki

 Wapendwa katika Bwana,

 Nachukua nafasi hii kuwashukuru ninyi wote kwa jinsi mlivyoipokea na kuanza kuifanyia kazi barua yangu ya kuwaomba mchango kwa ajili ya kulipa deni la Dayosisi.

 Najua kuwa wale waliotufikisha hapa wanaandika barua wakidai kuwa Dayosisi hii haidaiwi chochote lakini endeleeni kuwapuuza na maneno yao kwa kuwa deni la Dayosisi liko wazi mahali pote.

 Nimeona wengi mmeanza kutoa michango yenu kwa nguvu kubwa endeleeni hivyo ili turudishe heshima ya Dayosisi yetu. Nahimiza tuendelee kuchanga na pale unapotoa ama kuingiza Bank taarifa zako zifike kwa Mchungaji wako wa Usharika ili kuweka kumbukumbu zako vizuri.

Taarifa hiyo kwa mwezi April imeonesha Usharika husika umetoa kiasi gani, jumla ya kiasi katika Usharika unatakiwa kutoa kiasi gani kulingana na barua walizopokea na mwisho taarifa hiyo inaonesha kiasi kinachobaki. Hata hivyo taarifa hiyo ya mwezi April imeonesha kua Dayosisi nzima katika mwezi April imechanga kiasi cha TSh.14,335,200/= kilichosaidia kupunguza  sehemu ya madeni mbalimbali.

Mungu aendelee kuwabariki ninyi wote kwa jinsi mnavyoendelea kujitoa ili kurudisha heshima ya Dayosisi yetu.

 “Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, nitakushauri jicho langu likikutazama”, Zaburi 32:8.