Print

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs), Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewashukuru wanadayosisi na wote walioshiriki katika maombi ya kumuombea mwenzi wake Mwl. Mary Mbilu katika kipindi chote cha kuugua kwake.

Ametoa shukrani hizo katika Ibada maalumu ya kumshukuru Mungu kwa kumponya na kumvusha katika kipindi kigumu cha kuugua kwa mwenzi wake na kusema kuwa maombi na sala za wanadayosisi ndugu jamaa na marafiki yamekuwa faraja kwao na kuwaomba kuendelea kuikumbuka familia hiyo katika maombi.
Katika hatua nyingine Askofu Dkt. Mbilu amewahimiza waumini na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika zoezi la sensa ya watu na makazi ambayo inatarajiwa kufanyia mwezi Agosti,2022 kwa lengo la kupata takwimu sahihi kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla huku ikiongozwa na kauli mbiu isemayo: SENSA KWA MAENDELEO, JIANDAE KUHESABIWA

 


Aidha kwa upande wake Mwl. Christopher Mwakasege ambaye ndiye aliyehubiri neno la Mungu katika Ibada hiyo maalumu ya Shukrani iliyofanyika Kanisa Kuu Lushoto, amewataka waumini kujijengea tabia ya kumshukuru Mungu kwa matendo makuu anayowatendea kwani kwakufanya hivyo wanampa nafasi Mungu kuzidi kutenda miujiza juu yao.


Ibada hiyo ya Shukrani pia imehudhuriwa na Askofu Mstaafu wa KKKT-DKMs Mzee Joseph Jali,viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Kalisti Lazaro,Diwani wa Lushoto Mjini,Mkurugenizi wa Halmalmashauri ya Lushoto pamoja na ndugu jamaa na marafiki kutoka ndani na nje ya Dayosisi.