
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amepokea ugeni maalum kutoka Vyuo vikuu vitano ambavyo ni, Muhimbili (MUHAS), KCMC/KCMU,Chuo cha Kenyata kilichopo Kenya,Chuo cha Protoria cha Africa ya Kusini na Chuo kikuu cha Leibniz kilichopo Hannover Ujerumani, uliokuja kwa lengo la kutembelea vituo mbalimbali vinavyomilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ili kuanzisha umoja wa Vyuo hivyo na Taasisi ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) kwa madhumuni ya kuanzisha kozi ya lugha na mawasiliano ( Speech and language therapy).

Askofu Dkt. Mbilu amesema kuwa anatambua umuhimu wa kuanzisha uhusiano na Vyuo hivyo vikuu kwa lengo la kuanzisha mitaala mbalimbali pamoja na kufanya tafiti ambayo itasaidia kukuza taasisi hiyo changa ya KOTETI na kutengeneza mazingira rafiki yatakayowezesha Taasisi ya Elimu KOTETI kuingia kwenye mradi wa Lugha na mawasiliano.

Kwa upande wake Dkt Enica Richard ambaye ni mkuu wa chuo cha MUHAS amesema kuwa, ni wakati wa Vyuo na Taasisi vinavyotoa kozi maalum kuungana na kukua kwa pamoja ili jamii ipate wataalam waliopikwa vizuri na kutatua changamoto inayoikabili jamii kuanzia ngazi ya watoto hadi watu wazima.

Nae Mwl.Afizai Vuliva ambaye ni mtaalamu wa Lugha na mawasiliano kutoka KCMC amesema kuna umuhimu mkubwa wa taaluma hiyo kwa jamii na pia ameonesha tafiti aliyoifanya sambamba na kuelezea faida zake huku akisema tayari KOTETI ina vifaa na mazingira rafiki ya kujifunza kwa vitendo kutokana na uwekezaji uliofanywa na Dayosisi ya kua na vituo ambavyo vinarahisisha utendeji kazi katika tafiti mbalimbali.

Ziara ya wataalamu hao ni ya siku tatu ambayo itahitimishwa tarehe 9/6/2023 na watatembelea vituo mbalimbali vinavyomilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.