
Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Mhandisi Robert Kitundu amewataka Wakristo wa KKKT kuendelea kuliombea Kanisa na kulisogeza mikononi mwa Mungu ili liendelee kudumu katika Umoja na upendo wa kweli.

Katibu Mkuu huyo ameyasema hayo leo tarehe 09/07/2023 kwenye Ibada ya Jumapili iliyofanyika KKKT-Dayosisi ya Mashariki na Pwani Jimbo la Magharibi Usharika wa Kimara ambapo pamoja na kuliombea Kanisa amewasihi Wakristo kutunza Ulutheri katika kumtukuza Mungu.

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt.Msafiri Joseph Mbilu ambaye yupo katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi anayoifanya KKKT-DMP ni mmoja wa walio shiriki katika Ibada hii.

Mchana wa leo Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu atakuwa na mkutano na Wakristo wote wanaotokea KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Lushoto, Tanga pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo waishio Dar es Salaam kuanzia saa 9:00 Alasiri. Mkutano huu utafanyika kwenye ukumbi wa mikutano KKKT - Mbezi Beach.
