KATIKA PICHA: Ibada ya Jumapili ya tarehe 15/10/2023 kutoka Jimbo la Tambarare Usharika wa Muheza. Ibada hii iliongozwa na Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ilikuwa na tendo la kuwabariki vijana wa Kipaimara. Pamoja na hayo Vijana hao waliobarikiwa wamemshukuru Mhashamu Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu kwa kufundishwa neno la Mungu kwa kipindi cha miaka miwili huku wakitoa pongezi kwa kazi mbalimbali za maendeleo zinazofanyika ndani ya Dayosisi chini ya uongozi wa Baba Askofu Dkt. Mbilu.

“Mhashamu Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu, sisi vijana wako tunamshukuru sana Mungu kwa kutuwezesha kufikia siku hii ya leo ya tarehe 15/10/2023. Tunapenda kukushukuru wewe pamoja na Ofisi yako kwa ujumla, kwa kazi mbalimbali mnazozifanya katika Dayosisi yetu Mungu awabariki sana.

Siku hii ya leo tunayofuraha kubwa ya kuhitimisha mafundisho yetu ya Kipaimara tuliyopata kwa muda wa miaka miwili, ambayo yametuimarisha vyema kuifahamu imani yetu ya Kikristo, kwa kujifunza Biblia na kitabu cha pokea chapa ya Kristo. Hakika tumepata msingi mzuri sana katika maisha yetu.

Mhashamu Baba Askofu sisi tunaobarikiwa leo tuna kushukuru na kukupongeza sana, tumetambua jitihada zako kubwa za kuiwezesha Dayosisi yetu kumhudumia mwanadamu kiroho, kimwili na kiakili, hivyo basi tunaungana nawe katika harakati za kulipa deni kubwa linalo ikabili Dayosisi. 
Kwa kutambua jitihada zako tunaungana nawe na wanadayosisi wote kwa kutoa kiasi cha Tsh: Laki tatu (300,000)” Walisema watoto hao, ambapo mara baada ya kuungwa mkono na wazazi, walezi pamoja na watu mbalimbali walioshiriki katika Ibada hiyo jumla ya kiasi cha Tsh. 824,950 kilikusanywa na kuelekezwa katika ulipaji wa deni la Dayosisi.
