
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amewataka Wazazi na Walezi wanapo upokea mwaka Mpya wa 2024 kuendelea kuwalea Watoto wao katika maadili mema kwani malezi bora ndiyo msingi wa kumsaidia Mtoto kutimiza malengo yake ya mbeleni.
Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo mara baada ya Ibada ya siku ya mwaka Mpya wa 2024 iliyofanyika katika Jimbo la Kusini Usharika wa Vuga iliyotanguliwa na uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ofisi ya Usharika na kusema kuwa katika jamii ya sasa kumekua na ongezeko la mmomonyoko wa maadili hivyo kuwataka wazazi na walezi kusimama katika nafasi zao ili kuwalea watoto na vijana katika maadili mema pamoja na kukemea maovu.
Katika hatua nyingine Askofu Dkt. Mbilu amewataka watumiaji wa vyombo vya usafiri kuhakikisha wanafuata sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizokua na sababu.
Sehemu ya Salamu za Mwaka Mpya 2024 za Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, kwa Wakuu wa Majimbo, Wachungaji, Mashemasi, Wainjilisti, Wakristo wote, KKKT-DKMs.
Wapendwa katika Bwana "HERI YA MWAKA MPYA" Ninyi wote mtaungana nami kuwa tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu wetu kwa jinsi alivyotulinda na kututunza kwa mwaka mzima huu wa 2023. Tukiutazama mwaka 2023 wote tunatambua kuwa tunayo mengi ya kumshukuru Mungu ambayo hayawezi kuhesabika wala kuchunguzika. Ndipo tunapoungana na mwimbaji wa Zab. 116:14 akisema "Nimrudishie BWANA nini Kwa ukarimu wake wote alionitendea? Nitakipokea kikombe cha wokovu; Na kulitangaza jina la BWANA" Ninaleta wito kwenu ninyi wote kumshukuru Mungu kwa wema wake kwetu na kukubali kubeba wajibu wa kuendelea kumtumikia kwa vipawa vingi alivyotupa na mali nyingi alizotujalia. Kwa barua hii ya Salam za Mwaka Mpya nawiwa kuleta kwenu mambo machache kama ifuatavyo: 1. Kwanza napenda kuwashukuru ninyi wote kwa jinsi mlivyoitikia wito wa kulipa Deni la Dayosisi yetu. Asanteni kwa moyo wenu wa kujitoa kwa kazi ya Bwana. Deni linaendelea kupungua kwa kasi kubwa na ipo siku litamalizika kabisa. 2. Nachukua nafasi hii kuwaletea taarifa ya uchangiaji wa Deni kwa Mwaka 2023. Katika Mwaka 2023 tumefanikiwa kuchangia Deni kama ifuatavyo: i) Barua ya Askofu kwa Washarika wote tumekusanya Sh. 251,271,900 ii) Sh. 30,000 kila Msharika tumekusanya Sh. 298,595,800.00
iii) Harambee ya Dar es Salaam Fedha Taslim ni Sh. 63,630,000.00 Ahadi Sh. 371,368,000.00 Jumla. 434,998,000 iv) Harambee ya Tanga Fedha Taslim ni Sh. 64,697,000.00 Ahadi Sh. 78,505,800.00 Jumla. 143,202,800.00 v) Siku ya Kuhitimisha uchangiaji wa Sh. 30,000 Korogwe Fedha Taslim Sh. 20,962,100.00 Ahadi Sh. 676,000.00 Jumla. 21.638,100.00 vi) Misaada ya Marafiki wa Ujerumani Sh. 26,166,000.00 vii) Wanadayosisi Waishio nje ya Dayosisi Sh. 14,182,000.00 viii) Vituo vya Dayosisi Sh. 16,665,000.00 Jumla Kuu kwa Mwaka 2023 tumekusanya Tsh. 756,169,800.00 Deni tuliloanza nalo Januari 2023 Tsh 6,451,271,900.00 Deni lililolipwa ni Tsh 756,169,800.00 Deni tunaloanza nalo Januari 2024 ni Sh. 5,695,102,100 (Bilioni Tano Milioni Mia Sita Tisini na Tano Mia Moja na Mbili Elfu Mia Moja tu) 3. Kikao cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi kilichokaa hivi karibuni kimeweka maazimio kuwa: Tunawapongeza Washarika wote kuwa Deni limepungua toka Billion 7.6 na kufikia Billion 5.7 Tuwe na mkakati kabambe wa kumaliza Deni hili ndani ya miaka miwili yaani 2024 na 2025.
Kila Usharika uunde Kamati maalum ya Deni kuanzia kwenye mitaa hadi kwenye ngazi ya Usharika. Viongozi wa Sharika wataunda Uongozi wa Jimbo na Viongozi wa Majimbo wataunda Uongozi wa Kidayosisi. Wachungaji wote wasimamie zoezi la uundwaji wa Kamati hizi na kuwasilisha majina ya Viongozi kwa Wakuu wa Majimbo. Viongozi kwa kila ngazi watakuwa wanne yaani Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na Mtunza Hazina. Kamati hizi ndizo zitakazoratibu na kusimamia uchangiaji wa Deni hili kuanzia kwenye Mtaa, Usharika, Jimbo na Dayosisi. Kamati ya Kidayosisi itaratibu na kusimamia michango iliyotolewa kila mwisho wa Mwezi na itasimamia ulipaji wa Deni kila mwezi na kutoa taarifa. Kila Msharika wa Dayosisi anaombwa kuchangia kiasi cha Sh. 10,000 kwa mwezi. Kiwango hiki ni sawa na wastani wa Sh. 2,500 kwa Juma moja. 4. Napenda kuwatangazia kuwa Mwaka 2024 ni Mwaka wa Wanaume katika Dayosisi yetu. Ninawasihi Wanaume mahali popote walipo wajipange kuupokea Mwaka huu, kuandaa mpango kabambe wa kuwafikia wanaume wote wa Dayosisi hii. 5. Neno la Mwaka 2024: Ninayo furaha kuwatangazia kuwa Neno Kuu la Mwaka 2024 ni lile lile la mwaka 2023 kutoka Ayubu 22:21 "Mjue sana Mungu ili uwe na Amani, ndivyo mema yatakavyokujia". Ninawakaribisha wana Sanaa na wataalam mbalimbali wa muziki kutunga nyimbo, Mashairi, michezo ya kuigiza nk. wakitumia neno hili.
Nawatakia Baraka za Mungu katika mwana Mpya 2024.
HERI YA MWAKA MPYA!
Pendoni mwa Kristo,
KKKT-DAYOSISI YA KASKAZINI MASHARIKI
Mch. Dkt Msafiri Joseph Mbilu
ASKOFU