NENO KUU: JIANDAE KWA HUKUMU YA MWISHO
NENO LA MAHUBIRI: Mathayo 25:14-30
UTANGULIZI
Leo ikiwa ni jumapili ya pili (2) kabla ya kuingia katika kipindi cha MAJIRIO, majira ambayo wakristo wote ulimwenguni wanayaangalia mambo makubwa mawili 1. Kukumbuka ujio wa kwanza wa Bwana Yesu hapa ulimwenguni ambapo miaka zaidi ya 2000 iliyopita alizaliwa na kuleta ukombozi kwa kila mtu aliyemuamini na wanaoendelea kumuamini hata sasa. 2. Jambo la pili ambalo sisi wakristo tunaliangalia katika majira haya ni maandalizi yetu kwa ajili kumpokea Bwana Yesu katika ujio wake wa pili, ambapo analijia kanisa lake katika hukumu ya mwisho.
Sasa ukisoma sura ya 24 ya injili hii, mstari 3 na kuendelea utaona Bwana Yesu anawafundisha wanafunzi wake juu ya dalili na ishara za siku za mwisho namna zitakavyokuwa, anawaambia watakavyoanza kuona watu kijiweka kwenye daraja la Kristo yaani kunifananisha na Kristo, vita (taifa na taifa kupigana), chuki na usaliti miongoni mwa wateule, manabii wa uongo, upendo wa wengi kupoa na mwisho kabisa chukizo la uharibifu lile lililotabiriwa na Nabii Isaya kusimama katika patakatifu mambo kama haya yakianza kutokea basi wajue kuwa ule mwisho umekaribia sana na wakati wowote Bwana Yesu atalijia kanisa lake.
Kwa kuzifahamu ishara na dalili za namna siku za mwisho zitakavyokuwa, tunatakiwa kuwa tayari wakati wote japokuwa hatujui siku wala saa halisi ambayo Bwana Yesu atakuja kulichukua kanisa lake. Na hapa ndipo yanapoibuka maswali haya muhimu (Je! Ni kitu gani tunatakiwa kukifanya pindi tunapoendelea kumngoja Bwana Yesu? Je! Tukae tukijibweteka tu bila kufanya kitu chochote?) majibu ya maswali haya yanajibiwa na kifungu tulichokisoma ambacho ndio msingi wa somo letu la leo kwamba tunatakiwa kujiandaa kwa ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa kuwa mawakili waaminifu kwa rasilimali na uwezo ambo kila mmoja wetu amepewa na Mungu.
SOMO LENYEWE
Na Bwana Yesu anatufundisha jambo hili muhimu kwa kutumia mfano wa TALANTA (Kwa nyakati hizo neno talanta lilitumika kuonyesha thamani ya fedha). Na katika mfano huu “TALANTA” ina maanisha rasilimali na vipawa mbali mbali ambavyo Mungu amempa kila mmoja wetu ili tuvitumie kwa ajili ya utukufu wake. Mchambuzi mmoja wa injili ya Mathayo aliyeitwa John Charles anasema; “Kitu chochote ambacho tunaweza kutitumia kwa ajili ya kumtukuza Mungu basi hicho kitu huitwa “TALANTA” na anatoa mfano wa talanta kuwa ni kama vile; vipawa vyetu, ushawishi wetu, fedha zetu, maarifa yetu, afya zetu, nguvu zetu, muda wetu, Mawazo na fikra zetu, uwezo wetu wa kiakili, kumbukumbu zetu na vitu vingine vinavyofanana na hivyo. Hivyo vyote ni sehemu ya talanta ambazo Mungu amewapa wanadamu ili wazitumie kwa ajili ya kuujenga utukufu wa Mungu hapa duniani."
Sasa kwa kujibu lile swali la kwanza (Je! Ni kitu gani tunatakiwa kukifanya pindi tunapoendelea kumngoja Bwana Yesu?) ni kwamba kila mmoja wetu anatakiwa asibweteke/asikae kwa hasara bali awe na juhudi kubwa katika kufanya kazi ya kumtumikia Mungu kupitia “TALANTA” ambayo Mungu amempa (Tena hutakiwi kuifanya kazi ya Mungu kwa kulalamika au kuitilia mashaka).
Fanya kazi ya Mungu bila kuchoka huku ukisubiri kurudi kwake ukitambua kuwa atakaporudi utatoa hesabu ya namna ulivyomtumikia.
Bwana Yesu kwa kutaka wanafunzi wake tukiwemo sisi tuelewe vizuri somo hili la kujiandaa kwa ajili ya hukumu ya mwisho na namna tutakavyotakiwa kutoa hesabu ya utumishi wetu anatoa mfano huu muhimu wa mtu Tajiri ambaye alipanga safari na kabla hajasafiri aliwaita watumwa wake watatu na kuwapa mali zake kwa kadri ya uwezo wa kila mmoja ili wazizalishe ili pindi atakaporudi aweze kupata na faida yake.
Mtumwa wa kwanza alipewa talanta tano (5), mtumwa wa pili alipewa talanta mbili (2) na mtumwa wa mwisho alipewa talanta moja (1) kila mmoja alipewa kulingana na uwezo wake. Yule mtumwa wa kwanza alizifanyia kazi talanta zaka tano na kuzizalisha mara mbili yake na mtumwa wa pili hivyo hivyo, lakini yule mtumwa wa tatu baada ya kuona amepewa talanta moja basi akaichukua talanta hiyo na kwenda kuifukia aridhini.
Ndugu zangu, kwenye mfano huu yapo mambo mengi ya kujifunza, na mimi nimechukua machache:
1. Kumbe tunatakiwa kujua kuwa vitu vyote tulivyo navyo si vyetu bali vinatoka kwa Mungu.
2. Jambo la pili, tunatakiwa kujua kuwa Mungu ametupa vile tulivyo navyo kila mmoja kulingana na uwezo wake.
Hapa tunatakiwa kuwa makini sana kwani wakati mwingine tumenung’unikia Mungu na kumuona kuwa pengine ana upendeleo kwa sababu tu labda sisi ametubariki kidogo na wengine amewabariki zaidi (sisi ni maskini na wengine ni matajiri) na wakati mwingine wale waliobarikiwa vingi wamewadharau wale waliobarikiwa vichache na kuwaona kuwa si watu wa maana.
3. Jambo la tatu tunalojifunza ni swali ambalo tunatakiwa sisi sote kujiuliza: Je unakifanyia nini kile ambacho Mungu amekupa?
Katika somo hili Bwana Yesu anatakata kutufundisha juu umuhimu wa kuwa watumishi waaminifu kwake, kwa kufanya kazi yake hapa duniani tena kwa kufuata maelekezo na vipawa alivyotupa. Kama ambavyo anawaelezea wale watumwa wawili yule wa kwanza na wa pili ambao baada ya kupewa talanta zao walikuwa waaminifu tena kwa hekima walizifanyia kazi talanta zao na kuzizalisha mara mbili zaidi na baada ya tajiri wao kurudi alifurahi sana kwa kazi yao njema.
Ndugu zangu, siku zote Mungu wetu anatutegemea tuwe waaminifu sana kwa kile ambacho ametupa na tena tunapaswa kukumbuka kuwa kanuni ya Mungu ni hii UKIPEWA VINGI UTADAIWA VINGI VILE VILE, UKIPEWA KIDOGO UTADAIWA KIDOGO!!! Na mwisho kabisa UKIWA MUAMINIFU KWA KIDOGO, MUNGU ATAKUAMINI KATIKA MAMBO MAKUBWA PIA!
Yule mtumwa wa tatu, Mtumwa mbaya, mlegevu/mvivu na asiyemwaminifu. Yeye kwa kuwa alifukia talanta yake hakuwa na faida yoyote aliyompatia baada ya kurudi kutoka safarini, bali alimuambia Bwana wake maneno haya “Nalitambua yakuwa wewe u mtu mgumu wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako kwenye ardhi; tazama unayo iliyo yako.”
Na hapa Bwana Yesu anataka kutufundisha jambo kubwa kuwa, turidhike na kile ambacho Mungu ametupatia na bila manung’uniko wala kumfikiria vibaya Mungu wetu kuwa labda ametudharau na kutuona hatufai kwani Mungu wetu anatuwadhia yaliyo mema kuliko sisi tunavyowaza. Kwenye habari hii tunaona kuwa yule Tajiri alichukizwa sana na tabia na maneno la mtumwa huyu asiyemuaminifu na akamwambia; “Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoa riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.” Na kisha akaagiza mtumwa yule asiyemuaminifu anyang’anywe hata ile talanta moja aliyokuwa nayo na kisha apewe yule mwenye talanta kumi. Kwa maana imeandikwa “Kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu hata kile alicho nacho atanyang’anywa.” Na tena adhabu hiyo haikutosha yule Tajiri akaagiza wamkamate yule mtumwa asiyemwaminifu na kumtupa katika giza la njeambapo ndipo kutakuwapo kilio na kusaga meno.
Ndugu zangu kumbe kitendo chakutokuvitumia vipawa (Talanta) ambavyo Mungu ameviweka ndani yetu kwa kazi yake ni jambo baya na lisilokubalika mbele za uso wa Mungu na mwisho wa siku kila mmoja wetu atatakiwa kutoa hesabu mbele ya kiti cha hukumu.Ndugu zangu Mungu anaendelea kutoa wito kwetu hata leo hii akiendelea kutukumbusha juu ya wito mkuu wa kumtumikia kupitia vipawa (Talanta) alizotupa. Hebu tumtumikia pasipo kuchoka wala manung’uniko huku tukiukomboa wakati kwani muda umeenda sana na dalili na ishara zote ambazo Yesu Kristo aliwafundisha wanafunzi wake tayari zimeshatokea. TUFANYE KAZI KUNGALI MCHANA KABLA GIZA HALIJAINGIA MAHALI AMBAPO HATUWEZI KUFANYA KAZI TENA!!!
Mungu alibariki Neno lake!
Ameen!!
Mchg. Thadeus A. Ketto
KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki