Print

Ndugu zangu wapendwa,

Ninawasalimu katika Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo!

SALAAM ZA SIKUKUU YA KRISMASS, 2020

Isaya 9:2 “Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.”

Heri ya Krismas!

 Tunamshukuru Mungu Baba yetu wa Mbinguni aliyetujalia sisi sote kuiona Krismass ya mwaka huu 2020.

 Sikukuu ya Krismass, ni sikukuu kubwa inayosherehekewa na watu wengi Ulimwenguni pote. Siku hii ni sikukuu ambayo sisi Wakristo tunapokea zawadi kubwa kutoka kwa Mungu mwenyewe kwa kumtoa mwanawe mpendwa Yesu Kristo azaliwe katika ulimwengu huu kwa ajili ya ukombozi wetu.

Nabii Isaya alitoa unabii wake unaokaza ujio wa Nuru Kuu ulimwenguni, nuru itakayolishinda giza. Kwa vyovyote Nabii aliishi wakati ambao watu wamesongwa na giza nene lisiloweza kuepukika. Giza la kukandamizwa kiimani, kisiasa na kijamii. Katikati ya giza nene Isaya anakuja na ujumbe wa matumaini kuwa Nuru Kuu itakuja na itawaangaza wote. Kwa vyovyote ilikuwa vigumu kwa wasikilizaji wa Isaya kuamini kuwa hiyo nuru kuu itakuja lini. Jinsi walivyozungukwa na uvuli wa mauti ilikuwa vigumu kuamini ujio wa nuru hiyo.

Kwa kuja kwa Yesu Kristo ulimwenguni, unabii huu unatimia. Nuru kuu imeingia ulimwenguni, uvuli wa mauti umetokomezwa.

Sisi tunaomwamini Yesu Kristo tufungue mioyo ili tuipokee nuru hii katika maisha yetu. Nuru hii ikaondoe giza linalotanda katika maisha yetu, katika mioyo yetu.

Nawatakia Krismas Njema,

Ni mimi Mtumishi mwenzenu Shambani mwa Bwana!

Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu

ASKOFU MTEULE – KKKT –DKMs