Print
Baba mzazi wa Askofu wa KKKT - Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt. Alex Gehaz Malasusa, Mch. Gehaz Malasusa amefariki dunia usiku wa kuamkia tarehe 8, Disemba 2021 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.
Taarifa ambayo imetolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo imeeleza kuwa imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kutwaliwa kwa mtumishi huyo ambaye katika kipindi chake cha utumishi alifanya kazi ya Mungu kwa unyenyekevu mkubwa katika maeneo mbalimbali ya Dayosisi, wakati huo ikiwa bado ni Sinodi ikihusisha mikoa ya Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
Marehemu Mch. Gehazi Malasusa alibarikiwa kuwa Mchungaji mwaka 1967 katika Kanisa Kuu la Azania Front na pia mwaka 1970 alienda kujiendeleza kimasomo nchini Marekani, akisomea shahada ya Theolojia na uongozi na akatumika katika Sharika mbalimbali ikiwemo Magomeni, Kurasini, Temeke, na Mtaa wa Mkulazi.
Akiwa Mchungaji wa Usharika wa Temeke, alianzisha mitaa ya Vetenari, Yombo Kuu, Vituka na Tandika, ambayo sasa ni Sharika kubwa.
Katika utumishi wake pia alitumika kama mwalimu wa somo la dini katika shule za sekondari na vyuo vilivyoko mkoa wa Morogoro.
Alipata kusema kuwa wito wa kumtumikia Mungu aliupata, baada ya kumuona baba yake mzazi akitumika shambani mwa Bwana kama Mwinjilisti
Mipango ya mazishi inaendelea nyumbani kwa marehemu Kijichi jijini Dar es Salaam na tutaedelea kutoa taarifa zaidi.

"Naye atafuta kila chozi katika macho yao,wala mauti haitakuwepo tena,wala kilio, wala maumivu hayatakuwepo tena, kwa kuwa mambo ya kwanza  yamekwisha kupita " UFUNUO 21:4.

 Uongozi wa KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki unatoa pole kipekee kwa Askofu wa KKKT - Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mch Dkt. Alex Gehaz Malasusa, familia, ndugu, jamaa na marafiki popote pale walipo. 

BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe.