Print

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amesema kuwa hana mashaka na kazi inayoendelea ya ujenzi wa Kanisa jipya katika Usharika wa Mombo kutokana na kasi na mwenendo mzuri wa ujenzi wa Kanisa hilo.

Ameyasema hayo leo tarehe 18/04/2022 kwenye Ibada ya Jumatatu ya Pasaka iliyo ambatana na Harambee ya ujenzi wa Kanisa linalojengwa katika Usharika huo litakalokuwa na uwezo  wa kuingiza waumini wapatao 800 hadi 1000 kwa wakati mmoja huku Usharika huo ukiwa na wastani wa waumini wapatao 1,124.

Aidha Askofu Mbilu amesema kuwa Mkuu wa Kanisa la KKKT Mhe. Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo ataitembelea Dayosisi hii ndani ya mwaka huu na kupokelewa katika Usharika wa Bwiko na baadae Usharika wa Mombo ambapo ataweka jiwe la Msingi wa Kanisa hilo jipya huku akisema itakuwa ni mara ya kwanza kutembelewa na Mkuu  wa Kanisa toka miaka 20 iliyopita .

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Godfrey Tahona Walalaze ametoa wito kwa washarika wote kuendelea kushirikiana pamoja ili kupunguza na kumaliza madeni yanayoikabili Dayosisi sambamba na kuwashukuru Washarika wa Usharika wa Mombo na wana KKKT-DKMs kwa namna walivyo pokea vizuri barua ya Baba Askofu  juu ya ombi la kuchangia deni linaloikabili Dayosisi .

Hata hivyo amewatoa hofu waumini ambao wanania ya kuendelea kuchangia deni hilo na bado hawajapata barua zao kuwa zipo tayari na watazipata hivi karibuni ili kusaidia kupambana kumaliza  madeni hayo makubwa.

Katika harambee hiyo  iliyoongozwa na Baba Askofu Dkt Msafiri Mbilu jumla ya fedha taslimu iliyopatikana  ni Tsh 10,868,200, (Milioni kumi laki nane elfu sitini na nane na miambili) huku ahadi ikiwa ni Tsh 8,885,000,(Milioni nane laki nane na elfu themanini na tano) na kufanya pesa taslimu pamoja na ahadi kuwa Tsh 19,753,200.(Milioni kumi na tisa laki saba na hamsini na tatu elfu na mia mbili).

 ‘Je, huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? Basi sasa Bwana wa Majeshi asema zitafakarini njia zenu, Pandeni milimani mkalete miti,mkaijenge nyumba nami nitaifurahia,asema Bwana’. Hag. 1:4

 TAARIFA RASMI JUU YA UJIO WA MKUU WA KKKT, MHE. ASKOFU DKT. FREDRICK ONAEL SHOO ITATOLEWA HIVI KARIBUNI