Print

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Fredrick Shoo leo tarehe 27/7/2022 ameanza ziara rasmi ya kuitembelea KKKT–Dayosisi ya Kaskazini Mashariki itakayoambatana na kufungua na kuweka mawe ya msingi na kuongea na wana Dayosisi katika maeneo mbalimbali.


Akiwasili katika eneo la Bwiko Usharika Mteule wa Mkumbara Askofu Dkt. Shoo amepokelewa na mwenyeji wake Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu na wana Dayosisi na baadae aliwasili katika Usharika wa Mombo ambapo ameweka jiwe la msingi la Kanisa jipya na kuongoza Ibada ya Shukrani.


Akihubiri neno la Mungu katika Ibada hiyo kutoka kitabu cha Injili ya Mathayo 7:1-5 Mkuu wa Kanisa amekemea tabia za baadhi ya Wakristo kujihesabia haki na kuhukumu wengine hatua inayofifisha vipawa na karama za wengi katika kulijenga Kanisa la Mungu.


Mkuu wa Kanisa amesema kwakuwa hakuna mtu aliyekamilika kabisa hivyo waliowakristo waonyane kwa upendo bila kunyosheana vidole madhaifu ya wengine.


Mbali na hayo Mkuu wa Kanisa ameendesha harambee kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kanisa la Usharika huo wa Mombo na kuchangia kiasi cha shilingi 1,000,000.


Nae Askofu wa KKKT – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Dkt. Msafiri Mbilu amewapongeza wanadayosisi kwa namna walivyojitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Mkuu wa KKKT na kuwasihi kuendelea kujitokeza katika maeneo yote ya Majimbo ambapo Mkuu wa Kanisa atatembelea.


Kesho tarehe 28/07/2022 msafara wa Mkuu wa KKKT utaelekea Bumbuli, ambapo Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo ataendelea na ziara yake katika Jimbo la Kusini kwa kutembelea Usharika wa Bumbuli, Hospitali ya Bumbuli, Chuo cha Utabibu Bumbuli (BUCOHAs) na kisha ataelekea Lutindi ambapo atapata wasaa wa kuwasalimu Washarika wa Lutindi na kutembelea Hospitali ya wagonjwa wa akili Lutindi (Lutindi Mental Hospital).