Print

Msaidizi wa Askofu KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch. Michael Mlondakweli Kanju amewashukuru na kuwapongeza wachungaji wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa kazi nzuri wanazozifanya katika Sharika zao ikiwemo  mikutano na semina mbalimbali za neno la Mungu walizozifanya mwaka huu wa 2022.

Mch.  Kanju ametoa pongezi hizo leo tarehe 14/12/2022 ambapo amemuwakilisha Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kwenye ufunguzi wa mkutano wa wachungaji na mashemasi unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI)-Magamba.

Hata hivyo Mch. Kanju ameeleza kuwa Semina zitakazo fanyika mwakani (2023) katika sharika zitalenga mambo makuu mawili ambayo ni Injili na Ujasiriamali ili kuwawezesha waumini kusikia neno la Mungu na kupata elimu ya ujasiriamali itakayowasaidia katika kujiongezea kipato.

“Baadhi ya faida ambazo washarika watazipata baada ya kupata elimu hii ya ujasiriamari  ni pamoja na Ujira binafsi na nafasi za ajira kwa watu wengi , kupunguza umasikini miongoni mwa watu, kutumia ipasavyo rasilimali walizonazo, matumizi sahihi ya rasilimali watu, ujasiriamali pia hutoa mwanga katika kufanya na kuanzisha shughuli mpya, kukuza na kuendeleza uchumi katika nchi, kupunguza kiwango cha umasikini miongoni mwa watu, kupunguza tofauti katika maendeleo baina ya watu, mikoa pamoja nchi kwa ujumla”.