
Sehemu ya salamu za Pasaka za Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu
Nawasalimu katika jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo!
“Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbiko lao waliolala” 1 Wakorintho 15:20.
Wapendwa katika Bwana,
Pasaka ni tendo la ushindi kwa wote waaminio kupewa matumaini mapya na ya uhakika kuwa yapo maisha ng’ambo ya kaburi. Leo hii Wakristo wote ulimwenguni tunasherehekea kufufuka kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo ambaye nguvu ya kaburi haikuweza kumshika.
Mtume Paulo anaweka bayana kuwa, kwa kufufuka kwa Yesu tunao ushindi na uhakika wa maisha ya milele. Kristo mfufuka anakuwa limbuko lao waliolala na hivyo kutuletea ushindi dhidi ya mauti na kuzimu.
Mwaka huu tunasherehekea Pasaka katika dunia iliyojaa dhambi na uasi wa kutisha. yale maasi makubwa yaliyosababisha maangamizi ya Sodoma na Gomora yameanza kusikika nyakati hizi na kuonekana kuwa mambo ya kawaida hata ndani ya makanisa. Watu badala ya kuikimbia dhambi sasa wanaikimbilia dhambi na kuifanya ni kitu cha kawaida. Ukiyatazama haya yote utaona kana kwamba watu wamesahau ushindi aliouleta Yesu dhidi ya dhambi na mauti.
Nikiyatazama yote haya katika Pasaka hii ninawiwa kuleta wito huu kwetu sisi sote kama Kanisa kufanya yafuatayo:
- Kutubu mbele za Mungu atuondolee uovu wetu na kutuamsha kwa upya pale tulipoanguka
- Kusimama kwa pamoja kukemea dhambi na kuukataa uovu wa kila aina katika jamii
- Kumuomba Mungu atuepushe na maovu yanayotanda katika ulimwengu wa sasa
Tukiungana sote kuikemea dhambi kuanzia kwenye ngazi ya familia kwa njia ya malezi ya Watoto wetu, ngazi ya jumuiya, ngazi ya usharika na Dayosisi kwa umoja wetu tutashinda. Mungu atujalie kuendelea kuimarisha malezi bora ya Watoto wetu huku tukiitumainia nguvu ya ufufuko. Yesu aliyeshinda mauti na kuzimu atatushindia hata yale tunayoyaona ni magumu katika ulimwengu wa sasa.
Nawatakia ninyi wote Baraka za Mungu wetu katika Pasaka hii.
Kristo Amefufuka kweli kweli Haleluya.