
Ufunuo 14:13 “Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao”
Katibu Mkuu wa KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mwl. Julius Madiga kwa niaba ya Uongozi wa KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki anasikitika kutangaza kifo cha Mwj. Ridas Edward Jani kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 17/12/2023 nyumbani kwa marehemu Majengo Juu Hale.
Marehemu Mwj. Ridas Edward Jani alikuwa Mke wa Mchungaji Mstaafu Edward Jani. Katika uhai wake aliitumikia KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, katika nafasi ya Uinjilisti pamoja na Parishworker na alihudumu katika sharika mbalimbali za KKKT-DKMs ikiwemo Usharika wa Kana,Mgwashi, Amani na Mnazi.
Ibada ya Mazishi itafanyika Jumanne ya tarehe 19/12/2023 nyumbani kwa marehemu Majengo Juu Hale, saa tano Asubuhi na mwili wake utapumzishwa katika makaburi ya familia nyumbani kwa marehemu Majengo Juu Hale.
Uongozi unatoa pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa na marafiki popote pale walipo. BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na lihimidiwe.

Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amefika nyumbani kwa Mch. Mstaafu Edward Jani kumfariji pamoja na kuomba pamoja na familia ndugu na jamaa, na aliambatana na Msaidizi wake Mch Michael Kanju, Mkuu wa Jimbo la Tambarare Mch Frank Mtangi ,Wachungaji pamoja na watumishi wengine kutoka Ofisi Kuu ya KKKT-DKMs.