
KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, inayomiliki Hospitali ya Kilutheri Bumbuli (Bumbuli Lutheran Hospital) imeendelea kufanya maboresho katika Hospitali hiyo baada ya hivi karibuni kutoa mashine ya usingizi (Anesthesia Machine) pamoja na vifaa tiba vingine vya kisasa ambavyo vitasaidia kuendelea kuboresha huduma ya Afya Hospitalini hapo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Huduma za Jamii wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mwl. Afizai Elisa Vuliva, wakati akikabidhi mashine hiyo kwa uongozi wa Hospitali ya Bumbuli huku akiwataka kutunza mashine hiyo pamoja na vifaa vingine vilivyo pelekwa hospitalini hapo kutoka kwa Shirika la GIZ.
Pamoja na hayo Mkurugenzi Afizai amemshukuru na kumpongeza Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, kwa jitihada zake kubwa ambazo zimefanikisha kupatikana kwa mashine hiyo ya kisasa na Vifaa tiba vingine ambavyo vitakuwa msaada mkubwa katika hospitali hiyo. Mafanikio haya yanatokana na juhudi binafsi za Baba Askofu katika kuimarisha mahusiano mazuri na Taasisi ,Mashirika mbalimbali pamoja na Watu binafsi.
Mkurugenzi Afizai amelishukuru Shirika la GIZ (German Agency for International Cooperation) kwa kutoa Vifaa tiba kwa ajili ya kuboresha huduma ya Mama na Mtoto. Vilevile Mkurugenzi Afizai ameishukuru Serikali chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wa Taasisi za Dini katika kuihudumia jamii kwani kwa mahusiano mazuri yalipo kati ya KKKT-DKMs na Serikali pia, Hospitali ya Bumbuli imeendelea kupokea vifaa tiba kutoka Serikalini.
Kwa upande wake Daktari Mfawidhi wa Bumbuli Lutheran Hospital Dkt. Frank Lugaenda, mbali na kumshukuru Mkurugenzi wa Huduma za Jamii Mwl. Afizai amesema kuwa maboresho yanayofanywa katika Hospital yataongeza ufanisi katika utendaji wa kazi.
Naye Mtaalamu wa Dawa ya Usingizi Bw. Herman Mdamanyi mbali na kutoa shukrani kwa uongozi wa Dayosisi amesema kuwa mashine hiyo pamoja na vifaa vingine vya kisasa vilivyopelekwa Hospitalini hapo vitaboresha huduma ya Afya kwa sehemu kubwa.