Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, (KKKT-DKMs) Mch Dkt. Msafiri Josephu Mbilu, amewataka Wanaume wa KKKT- Dayosisi ya Kasikazini Mashariki kujitoa katika kukamilisha mipango na malengo waliyojiwekea katika mwaka wao huku akiwataka kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maadili mema  ikiwa ni pamoja na kukemea ndoa za jinsia moja,  huku akiwataka wanaume wa Dayosisi hiyo kijitoa na  kuhudhuria katika Ibada na kushiriki katika maswala mazima ya uimbaji wa kwaya.

Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo tarehe 17/03/2024 mara baada ya Ibada maalumu ya ufunguzi wa mwaka wa wanaume  iliyofanyika katika shule ya sekondari inayomilikiwa na Dayosisi hiyo Shule ya Seminari ndogo ya Bangala iliyohudhuriwa na Wanaume kutoka katika majimbo yote matano ya Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambapo amesema kuwa ni wakati sasa wa wanaume wa Dayosisi hiyo kuwa mstari wa mbele katika kulitumikia Kanisa na jamii kwa kuonyesha mambo yanayofaa na kukemea yale yasiofaa ili kuweza kupata baraka kutoka kwa Mungu.

“Tunamshukuru Mungu kwa siku ya leo kufungua mwaka wa wanaume kupitia Ibada hii maalumu ambayo imehudhuriwa na wanaume kutoka katika majimbo yote matano na tumekuwa na kwaya za wanaume kutoka katika kila Jimbo jambo ambalo linaonyesha Wanaume wa Dayosisi hii wamehamasika kuchukua majukumu yao na kuwa tayari katika kulitumikia Kanisa hivyo tunatarajia kuona mambo makubwa kutoka kwa Wanaume katika mwaka huu” alisema Askofu Dkt. Mbilu.

Ameongeza kwa kusema kuwa ni utaratibu wa Dayosisi hiyo kuhusisha makundi mbalilmbali katika Kanisa na kuyapa makundi hayo nafasi ya kulitumikia Kanisa, ambapo Wanaume wamepokea mwaka wao mara baada ya mwaka wa Wanawake wa Dayosisi hiyo kumalizika ambapo  wanawake wa Dayosisi hiyo nao waliweza kufanya mambo makubwa kwa kuweka alama mbalimbali katika Jamii na Kanisa.

 Sasa mwaka 2024 ni mwaka wa wanaume kaika Dayosisi hiyo na neno kuu linalo waongoza ni kutoka katika kitabu cha 1wafame 2; 2b “Basi uwe  hodari, ukajionyeshe kuwa mwanaume”.

Naye mwenyekiti wa wanaume wa Dayosisi hiyo Mwl. Raphael Abraham Mmaka amesema kuwa wamepokea wajibu huo kutoka kwa wanawake huku akiahidi kuyatekeleza mambo yote ambayo wanaume wamepanga kuyatekeleza huku akiahidi kuwahimiza wanaume wasiokwenda kanisani waamke na kuhakikisha wanakwenda kanisani ili kulifanya kanisa kuwa nanguvu na umoja.

Sehemu ya Risala ya Wanaume wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, kwenye uzinduzi wa mwako wao ilianza na Neno Kuu la Dayosisi. Mjue sana Mungu ili uwe na amani ndivyo mema yatakavyokujia. Ayubu 22:21 iliendelea kueleza kuwa. Mhashamu Baba Askofu, sisi wanaume tumeupokea Mwaka wa wanaume kwa moyo mkunjufu kwa sababu:-

  1. Sisi wanaume ni vichwa. Na kama sisi ni vichwa basi ni lazima kutenda kama vichwa sio katika familia zetu tu bali pia katika kanisa. Kitendo cha wewe baba Askofu kutangaza kuwa huu ni mwaka wa wanaume ni sawa na kutuambia kuwa sasa unataka kuona wanaume tukitenda kiume. Sisi tumelipokea hilo.
  2. Pili Dayosisi yetu inapitia katika wakati mgumu na hasa JANGA la madeni. Familia inapokumbwa na Janga lolote ndio wakati ambao baba wa familia anapaswa kusimama imara. Kuteuliwa kwa mwaka huu kuwa mwaka wa wanaume ni sauti ya baragumu inayoita wanaume kuamka na kupambana na JANGA la Madeni ambalo linaikabiri Dayosisi yetu. Sisi tumelipokea hilo.
  3. Kwa kuwa uchumi wa familia unapaswa kushikwa na wanaume hivyo kuteuliwa kwa mwaka wa wanaume ni ishara a Dayosisi yetu kuwa na nia ya kukuza uchumi wake wa ndani. Sisi tumelipokea hilo.
  4. Lipo tatizo la wanaume walio wengi kutoonekana kanisani. Hi inasababishwa na wanaume wengi kukosa utayari wa kutopenda Ibada. Mwaka wa wanaume utawakumbusha wanaume kurudi kanisani na kushiriki katika matukio mbalimbali ya Kanisa mwaka huu. Hili nalo tumelipokea.

Mhashamu Baba Askofu, baada ya kuteuliwa kwa mwaka huu kuwa ni mwaka wa wanaume, uongozi wa wanaume kwa kushirikiana na mratibu wa Jinsia na watoto katika ngazi zote tumefanya vikao kadhaa na kukubaliana mambo mbalimbali. Baadhi ya mambo havo ni:-

  1. Uzinduzi wa mwaka wa wanaume ufanyikie hapa katika shule ya seminari ya Bangala na tunakushukuru kwamba ulikubali hilo na kutujibu mara moja.
  2. Tumefanya maamuzi kuwa mwaka wa wanaume uende sambamba na uwekaji wa alama katika ngazi za Dayosisi, Jimbo na usharika. Katika ngazi ya Dayosisi tumekubaliana kuwa alama tutakayoiweka itakuwa ni kupaua jengo la ukumbi katika Shule ya Seminari ya Bangala.
  3. Kila Jimbo na kila Usharika itakuwa na miradi ya alama ambayo itafanywa kwa mwaka mzima. Miradi hiyo yote kwa Dayosisi nzima inatarajiwa kuwa yenye thamani ya zaidi ya Milioni 160. Hadi sasa tunaendelea kuratibu miradi hiyo kutoka katika kila usharika kupitia viongozi wa wanaume wa majimbo. Hivyo Baba Askofu jiandae kufungua miradi mingi mwishoni mwa mwaka wa Wanaume.
  4. Mradi huu pekee wa upauaji wa paa la Ukumbi ambao ni mradi wa alama wa Kidayosisi, unaouzindua leo, unatazamiwa kugharimu Jumla ya Tsh Milioni 80 hi ni kwa mujibu wa BOQ tuliyoletewa na Injinia wa Dayosisi. kiasi hiki kitagawanywa kwa wanaume katika majimbo kulingana na uwiano unaostahili.

Miradi ya majimbo pekee inatazamiwa kugharamu Jumla ya Tsh Milion 10 na miradi kutoka sharika zote inatarajiwa kufikisha jumla ya Tsh Milion 70. Hivyo kufanya miradi yote ya alama katika Dayosisi nzima katika mwaka huu wa wanaume kufikia Tsh Milioni 160. Miradi hii imegawanyika katika sehemu tatu. Miradi ya kiuchumi, miradi ya kimaendeleo na miradi ya kihuduma. Hata hivyo miradi mingi kati ya hiyo inatazamiwa kuwa ya kiuchumi ili kulisaidia Kanisa kiuchumi.

  1. Sisi kama wanaume tumekubaliana kuongeza nguvu katika kutoa sadaka maalum kupitia bahasha maalum za deni la Dayosisi. Tunaunga mkono mawazo yako kuwa Desemba mwaka 2025 uwe ni mwisho wa deni hili. Tumekubaliana kuingia kazini kama wanaume kuweka nguvu kubwa katika kutoa na pia kutafuta mbinu mbadala ya kutafuta fedha.

Mhashamu Baba Askofu, kwa kuzingatia mambo hayo hapo juu, tumependekeza tuwe na siku ya Askofu na wanaume. Siku ambayo Baba utapata nafasi ya kukutana na wanaume wa Dayosisi hii na kuzungumza nao wao kama vichwa, kubadilishana mawazo, kutafakari neno la Mungu na kufurahi pamoja kupitia michezo mbalimbali itakayofanyika siku hiyo.

Mhashamu Baba Askofu, leo tupo hapa kufanya uzinduzi wa Mwaka wa wanaume kwa sababu ya maono makubwa ya Baba Askofu Mstaafu Joseph Jali ya kuwa na shule ya Seminari hapa Bangala. Shule hi sasa ina zaidi ya miaka ishirini bila bwalo kukamilika. Sisi kama wanaume tumeona tuamshe upya maono ya Baba Askofu Mstaafu Joseph Jali angalau kwa kupaua ukumbi huu ambao utasaidia sana walimu na wanafunzi katika matendo ya kujifunza, mikutano, midahalo, mahafali na hata kwa ajili ya kulia chakula.

Mhashamu Baba Askofu, kwa kuwa leo ni uzinduzi wa Mwaka wa Wanaume, na kwa kuwa tumeamua kupaua paa la jengo hili kwa mwaka huu mzima. Sisi wanaume tunazindua kazi hii kwa Tsh milioni mbili, aidha tunaomba wenzetu mtuunge mkono. Ni matumaini yetu kuwa kiasi cha Tsh Milioni 80 kwa wanaume wa Dayosisi hii sio kikubwa kutushinda. Hivyo tuanze hapahapa kukipunguza kiasi hicho. Kisha tukitoka hapa tukatafute kiasi kilichobaki.

Mhashamu Baba Askofu, mwisho kabisa tunapenda tena kukushukuru sana wewe binafsi kwa jinsi ambavyo umetuunga mono na kwa jinsi ambavyo unaonesha jinsi unavyotegemea kundi hili la wanaume katika kuunga mkono kusukuma maendeleo na kazi za Dayosisi hii. Sisi tunakuahidi kuwa na wewe bega kwa bega hadi kuhakikisha tunaisogeza Dayosisi yetu hatua nyingine mbele zaidi ya mafanikio makubwa. Aidha tunamshukuru Baba Dean na Katibu Mkuu ambao kwa nyakati tofauti wamefuatilia kazi mbalimbali tulizoanza kuzifanya kama wanaume.

Kipekee tunamshukuru sana Mratibu wetu Mchungaji Neema Kamendu ambaye licha ya kuwa yeye ni mwanamke lakini amesimama na sisi kuhakikisha Kitengo hiki kipya kinaanza vizuri. Ni mama mwenye bidii na amekuwa karibu sana na sisi.

Pamoja na yeye tunawashukuru wakuu wa Majimbo wote kwa ushirikiano mkubwa walitupatia. Tunapenda kukiri wazi kuwa wakuu wa majimbo wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa michango yote iliyopangwa inachangwa na kutumwa kwa wakati. Sisi wanaume tunawategemea sana nyinyi wakuu wa Majimbo hasa ikizingatiwa kuwa kitengo chetu ni kipya. Ushirikiano wenu utasaidia kuleta mafanikio tarajiwa.

Hata hivyo kwa upekee wake tunapenda kumshukuru Kaimu Mkuu wa Jimbo la Pwani Mch. Emmanuel Mtoi ambave amekuwa mstari wa mbele kututia moyo wanaume na kuhakikisha kuwa tunasimama. Katika kikao cha kwanza cha wanaume ngazi ya Dayosisi kilichokuwa na uchaguzi wa kwanza wa wanaume Mchungaji Mtoi alisisitiza sana katika hotuba yake kuwa wanaume ni lazima tutende kiume.

Pia tunamshukuru Mkuu wa Jimbo la Tambarare Mch. Franki Mntangi ambaye amekuwa tayari kutukaribisha mara kwa mara kufanya vikao vyetu katika Usharika wa Korogwe. Katika kikao cha pili cha viongozi wa wanaume cha Dayosisi nzima kilichofanyika Korogwe Mchungaji Mntangi alisisitiza umuhimu wa wanaume kuanza vizuri na pia kutenda mambo yetu kwa juhudi ili kuzaa matunda.

Tunawashukuru pia wachungaji wote kwa jinsi ambavyo mmeonesha ushirikiano mkubwa huko sharikani. Kwanza kabisa kwa kuhamasisha na pili kwa ushiriki wenu hapa ambao unaonesha kuwa mpo tayari kushirikiana na sisi. Bila yenu kitengo cha wanaume hakiwezi kufanya mambo mazuri. Tunaomba muendelee kutupa ushirikiano huo. Tunawashukuru pia wanaume wote, viongozi wenzetu, wanakwaya kutoka Cathedral, na kwaya ya Tarumbeta kutoka Usharika wa Hengiti.

Mwisho kabisa tunawashukuru walimu na wanafunzi wa Shule ya Seminari ya Bangala kwa jinsi ambavyo wamehusika sana katika kusafisha eneo hili na pia kutupokea kwa upendo mkubwa. Kwa kweli wamefanya kazi kubwa licha ya uchache wao. Wanastahili pongezi sana. Sisi wanaume tunasema tumeanza na nyinyi na tutakuwa hapa hadi kazi ya kufunika ukumbi huu ikamilike.

Mhashamu Baba Askofu, kwa kumalizia risala yetu, sisi wanaume, tumependekeza tuwe na siku ya Askofu na wanaume. Siku ambayo Baba utapata nafasi ya kukutana na wanaume wa Dayosisi hii na kuzungumza nao wao kama vichwa, kubadilishana mawazo, kutafakari Neno la Mungu na kufurahi pamoja kupitia michezo mbalimbali itakayofanyika siku hiyo.

 

Tunakuomba uwetayari kwa siku hiyo kwa sababu utapata mengi kutoka kwa wanaume wa Dayosisi hii lakini nao wana hamu ya kusikia maono yako ili kwa pamoja tuijenge Dayosisi yetu. Basi uwe hodari, ukajionyeshe kuwa mwanamume. 1 Wafalme 2:2b.