Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (Lutheran World Federation “LWF”), Askofu Henrik Stubkjær amewasili nchini Tanzania tayari kuanza ziara yake ya siku 3 ya kuitembelea KKKT,ambapo amepokelewa na  na mwenyeji wake Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania  (KKKT) Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa .

 Hii ni ziara ya kwanza kwa Askofu Stubkjær mara baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa LWF katika mkutano Mkuu wa fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani uliofanyika Krakow, Poland mwezi Septemba, 2023.Katika ziara hii  Askofu  Stubkjær ameambatana na ujumbe wake akiwemo Makamu wa Rais kanda ya Afrika Mch. Dkt. Yonas Dibisa.

Pamoja na mambo mengine yatakayo zungumzwa katika  kulijenga Kanisa la Mungu ziara hii itampa nafasi Rais huyu kujitambulisha kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambalo ni moja ya Makanisa wanachama wa LWF atapata nafasi ya kuona maisha na kazi za Kanisa katika kuhubiri Injili, kumhudumia mwanadamu kwa ukamilifu wake kiroho, kiakili na kimwili.

Aidha atatembelea baadhi ya taasisi za KKKT kikiwemo Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, Shirika la Msamaria Mwema na taasisi zake ikiwemo Hospitali ya Kanda KCMC pamoja na kuona namna Kanisa linavyoendesha shughuli zake kupitia taasisi hizo.

Pia Askofu Stubkjær atashiriki mjadala wa matumizi ya nishati jadidifu (renewable energy) katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na mjadala hu baadhi ya viongozi na wataalam mbalimbali wa Kanisa, Serikali na wadau wengine wa maendeleo.