Msaidizi wa Askofu, KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Michael Mlondakweli Kanju amewashukuru Washarika wa Usharika wa Mgwashi na wanadayosisi kwa namna wanavyo endelea kujitoa kwa hali na mali kuchangia deni linaloikabili Dayosisi.
Msaidizi wa Askofu Mch. Kanju ametoa shukrani hizo leo tarehe 22/09/2023 kwenye Ibada iliyokuwa na tendo la kuwabariki vijana wa Kipaimara katika Jimbo la Kusini Usharika wa Mgwashi na kuongeza kuwa Dayosisi inalitambua deni na kwakuwa Kanisa linabaki kuwa chombo cha kutenda haki mahali popote hivyo wale wote wanaoidai Dayosisi watalipwa madai yao kwani Kanisa halina nia ya kudhurumu haki ya mtu yoyote.
Ameongeza kuwa kwa umoja na mshikamano uliopo deni hilo litakwisha na kuziacha mali za Dayosisi zikiwa salama,amewataka wana Dayosisi na wadau mbalimbali wa maendeleo ambao tayari wameingia kazini na kuonesha moyo wa kuchangia deni hilo kuwapuuza watu ambao wamekuwa wakiitumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kueneza habari za uongo kuwa Dayosisi haidaiwi.
Pamoja na hayo Msaidizi wa Askofu ameonesha kufurahishwa kwake na kazi za maendeleo zinazo fanyika katika Usharika wa Mgwashi ikiwemo ujezi wa Ofisi, Kanisa na namna vijana waliobarikiwa walivyo andaliwa, kwa kufundishwa imani ya Kikristo kwani kwa imani hiyo wamedhibitisha ubatizo wao na hawata yumbishwa na mafundisho potofu yaliyotanda katika jamii ambayo yanaweza kuwatoa uweponi mwa Mungu huku akiwasihi kuiishi na kuilinda imani yao.
Katika Risala ya vijana hao waliobarikiwa iliyosomwa mbele ya msaidizi wa Askofu Mch. Michael Kanju vijana hao wameeleza kuwa wameona juhudi mbalimbali zinazofanywa na uongozi wa Dayosisi,chini ya Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, katika kuiletea Dayosisi maendeleo na kupambana na deni hatarishi la Dayosisi, na kuungana na uongozi kwa kutoa jumla ya Tsh. 230,000 ambapo mara baada ya kuungwa mkono na wazazi, walezi pamoja na watu mbalimbali walioshiriki katika Ibada hiyo kiasi cha Tsh.730,000 kilipatika na kuelekezwa katika kulipa deni hilo linalo ikabiri Dayosisi.
Vijana hao wameongeza kuwa siku hii ya kubarikiwa kwao ni siku ambayo inaweka alama katika maisha yao na kwamba masomo waliyofundishwa hasa katika somo la uwakili yamewafanya kuwa nguzo muhimu katika ustawi wa Dayosisi na Kanisa la Mungu, Jumla ya Vijana wapatao 115 wamebarikiwa na mmoja kati yao alibatizwa.