Print

 Siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia zinaendelea katika mikoa yote Tanzania, ambapo leo tarehe 04/12/2020 Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa kushirikiana  na Kituo cha Watoto Wenye Ulemavu wa Akili (Irente Rainbow School) wametoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga.

ulimwengu ukiwa katika siku 16 za kuhamasisha kupinga ukatili wa kijinsia hususani kwa wanawake na watoto.Baadhi ya watu wenye mahitaji maalumu wilayani Lushoto Mkoani Tanga wameomba kuwekewa mazingira yenye uhakika wa kupata elimu bora, hali itakayo pelekea ushiriki wao kuwa mkubwa katika ngazi za maamuzi na uzalishaji mali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye semina iliyo jumuisha wazazi na walezi wenye watoto wenye mahitaji maalumu iliyoandaliwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa kushirikiana na Kituo cha Watoto Wenye Ulemavu wa Akili (Irente Rainbow School) wameiomba serikali na wadau wakati huu kuwawekea mazingira rafiki ya wao kupata elimu ya darasani na ya ujuzi wa kujitegemea.

Mratibu wa idara ya maendeleo ya Wanawake, Watoto na Jinsia wa CCT, Bi.Esther Muhagachi ameiasa jamii kuendelea kufichua ukatili wa kijinsi na kusisitiza kuwa kunyamazia vitendo hivyo vya ukatili ni ukatili hasa. Aidha Bi. Mhagachi amekishukuru kituo na uongozi wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMS) kwa kuwa na kituo hiki. Ameahidi ushirikiano na kituo na Dayosisi kwa ujumla katika jitihada zao njema za kuwafikia watu wenye mahitaji maalumu.

Mkuu wa kituo cha watoto wenye ulemavu wa akili Irente ambae pia ni meneja wa mradi wa kuimarisha maisha ya watoto na vijana wenye ulemavu katika milima ya usambara unaoendeshwa na Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMS), Mwalimu Lucy Mwinuka alimshukuru Mratibu wa idara ya maendeleo ya wanawake, Watoto na jinsia wa CCT kwa ajili ya semina hii ambayo imeamsha jamii juu ya ushiriki wao katika kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu katika ngazi ya familia, jamii na taifa. Amesema ipo haja ya kuongeza nguvu ya utoaji elimu ya ukatili wa kijinsia katika shule za msingi kwa sababu watoto wanayo nafasi kubwa ya kuelimisha kaya zao.