
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kama msimamizi wa mali za Dayosisi kupitia halmashauri Kuu ambayo yeye ni mwenyekiti wake amesema kuwa watahakikisha majibu ya zilipo fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya Dayosisi ambazo hazikutumika kama ilivyokusudiwa yanapatikana.

Katika kufanikisha hilo amesema kuwa watumishi mbalimbali ikiwemo wachungaji waliokuwa wakiwajibika kusimamia fedha hizo wataulizwa hata ikibidi kwa ukali.

Askofu Dkt. Mbilu amebainisha hayo leo Novemba 24,2021, kwenye Senta ya Missioni ng’ambo ya Mto Pangani-Sakura Jimbo la Pwani ambako ameongoza Ibada ya kipaimara na kuweweka jiwe la msingi la Kanisa . Jumla ya vijana 22 wamebarikiwa na wawili kati yao walibatizwakatika Ibada hiyo.Hata hivyo Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu amewapongeza washarika wa Missioni ng’ambo ya Mto Pangani-Sakura Kwa Kanisa zuri walilojenga ukilinganisha na Idadi ndogo ya washarika hao,Baba Askofu Mbilu ameongeza kuwa kwa kazi nzuri na zakuigwa zinazo endelea kufanyika katika Mission hiyo kupitia Halmashauri Kuu itakayo keti mwezi ujao atapeleka ombi la Mission hiyo kuwa Usharika teule.

Mapema siku ya jana Novemba 23,2021 Askofu Dkt. Mbilu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Jimbo la Pwani Mch. Thadeus A. Ketto, alikabidhi kiasi cha shilingi 8,000,000 Milioni nane ili kuunga mkono kazi ya ujenzi wa Kanisa la Mtaa wa Mwera na kiasi hicho kitatumika katika ununuzi wa bati za kuezekea Kanisa hilo.


Kwa upande wake msaidizi wa Askofu Mchungaji Michael Mlondakweli Kanju amewahimiza washarika kujiandaa na toleo maalumu (Sadaka) kwa ajili ya kukiwezesha Kituo cha Redio Utume kuweka busta itakayosaidia matangazo yake kusikika maeneo yote ya mkoa wa Tanga na uanzishwaji wa gazeti la Utume na hapo baadae televisheni. Toleo maalumu kwa ajili ya Redio Utume litatolewa jumapili ya Novemba 28, 2021.


