HABARI KWA UFUPI:Ibada ya Jumapili Sikukuu ya Watakatifu iliyoongozwa na neno kuu lisemalo sisi ni wenyeji wa Mbinguni, Ibada imefanyika leo tarehe 03/11/2024 katika Jimbo la Tambarare Usharika wa Muheza na kuongozwa na Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu.
 
Katika Ibada hii kulikuwa na tendo la kuwabariki Vijana 39 wa kipaimara na mmoja kati yao alibatizwa, ambapo vijana hao kwa kutambua changamoto ya Deni la Dayosisi linalosababisha mambo mengine ya kimaendeleo kutotekelezwa walitoa kiasi cha Tsh.300,000 kwa ajili ya kuchangia Deni hilo na baada ya hapo waliomba kuungwa mkono na Wazazi, Walezi na Wadhamini na baada ya kuungwa mkono kiasi cha Tsh.2,300,000 kilipatikana na kuelekezwa katika ulipaji wa Deni la Dayosisi.
 
Mmoja wa Vijana waliobarikiwa akisoma Risala kwa Baba Askofu Dkt. Mbilu,amesema kuwa wanamshukuru sana Mungu kwamba wameweza kukamilisha miaka miwili ya kufunzwa kateksimo ndogo ya Dkt. Martin Luther mafungu yote na pia wamepata nafasi ya kufundishwa na walimu wao neno la Mungu linalowataka kuishi maisha ya utakatifu hasa katika dunia hii yenye mabadiliko mengi hasa nyakati hizi za utandawazi.
 
Aliongeza kuwa wamejifunza mambo mbalimbali yanayo husiana na utumishi wao katika Kanisa kama vile uwakili wa kumtumikia Mungu kwa mali zao, kufanya kazi za mikono kama vile kufanya usafi katika maeneo ya Kanisa huku wakiwashukuru walimu wao kwa mafunzo waliyowapatia.
.
Kipekee Vijana hao waliobarikiwa wamemshukuru Baba Askofu Dkt. Mbilu kwa kutenga muda wake na kuwa pamoja nao katika siku ya kubarikiwa kwao jambo ambalo limewapa furaha kwa uwepo wa Baba Askofu.