Leo tarehe 04/12/2022 Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ameendelea na ziara yake nchini Sweden katika mji wa Uppsala (Cathedral) na ameshiriki kwenye Ibada ya kuingizwa kazini kwa Mkuu mpya wa  Kanisa la Sweden (The Church of Sweden), Askofu Dkt. Martin Modéus.

 Askofu Dkt. Mbilu ambaye pia amemuwakilisha Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo kwenye Ibada hiyo.

Mkuu wa KKKT anakupongeza sana kwa kuchaguliwa na kuingizwa kazini kuwa Mkuu mpya wa Kanisa la Sweden.Tunakutakia baraka tele za Mungu wakati huu wa kusimikwa kwako kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Sweden.

“Mungu wetu akupe nguvu na hekima zote  katika wajibu huu mkuu ulioupokea leo. Ni maombi na matumaini yetu kwamba urafiki na ushirikiano wetu wa muda mrefu na mzuri utaendelea chini ya uongozi wako. Sisi wa KKKT tunakuahidi kukuombea na kukupa ushirikiano wa kutosha.

Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso” (Zaburi 46:1).

Ibada hiyo imehudhuriwa na Maaskofu kutoka mataifa mbalimbali duniani ikiwemo, Norway, Finland, Denmark, USA, Tanzania pamoja na Ethiopia. Pia Katibu Mkuu wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (LWF), Katibu Mkuu wa Fungamano la Makanisa Duniani (WCC) pamoja na  Präses wa Kanisa la Westphalia (EKD) Annette Kurschuss  ni miongoni mwa watu walioshiriki katika Ibada hiyo.

 Askofu Martin Modéus alipata asilimia 59 ya kura katika uchaguzi  wa Askofu Mkuu uliofanyika tarehe 08/06/2022 hivyo amekuwa Askofu Mkuu mpya wa Kanisa la Sweden, akimrithi mtangulizi wake Askofu Antje Jackelen, ambaye alistaafu tarehe 30 Oktoba ya mwaka huu.

Askofu  Modéus anakuwa Askofu Mkuu wa 71 wa Kanisa hilo katika mlolongo usiokatika tangu Askofu Mkuu wa kwanza, Askofu Stephanus, mwaka 1164.