Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Alex Malasusa amesema kuwa ujio wa Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (LWF), nchini Tanzania Askofu Henrik Stubkjær utaendelea kuimarisha uhusiano uliopo na Makanisa ya Kilutheri  duniani katika kulitangaza neno la Mungu.

Askofu Dkt. Malasusa amesema hayo tarehe 16/04/2024 alipokuwa akifanya mazungumzo na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya KKKT yalipo Mkoani Arusha na kuongeza  kuwa, ni jambo la kumshukuru Mungu kwa Tanzania hususani KKKT kubapa bahati ya kutembelewa na Rais huyo ikiwa ni ziara yake ya kwanza mara baada ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo mwaka Septemba,2023, huku akieleza mchango wa   LWF ilivyohusika katika harakati za upatikanaji wa  Uhuru katika baadhi ya nchi barani Afrika.

Askofu Dkt. Malasusa ametuamia nafasi hiyo pia kuwapa pole watanzania waliopatwa na madhila ya mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini nakusema kuwa Kanisa la KKKT limeshaanza kutoa mchango wake na bado litaendelea kutoa msaada zaidi kwa waathirika hao, huku akimshukuru   Askofu Henrik Stubkjær ambaye ametoa kiasi cha Million 16,000,000 kuunga mkono juhudi za Serikali na Kanisa katika kukabiliana na majanga hayo.

Kwa upande wake Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani, Askofu Henrik Stubkjær amezindua mpango mkakati wa miaka mitano 2023-2028 wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira kinachomilikiwa na KKKT na kuahidi kuwa balozi wa Chuo hicho huku akikiri  kuvutiwa zaidi na namna KKKT inavyokua na kusema kuwa anatarajia  katika ziara yake ya siku tatu atajifunza zaidi namna KKKT inavyotekeleza mambo mbalimbali ikiwemo matendo ya huruma katika jamii (Diakonia).