Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewakumbusha Washarika wa Usharika wa Kana na Wakristo kwa ujumla, kuendelea kuomba neema ya Mungu iwaongoze katika kuomba kwa usahihi kama Kristo Yesu alivyo wafundisha wanafunzi wake katika Sala ya Bwana.

Askofu Dkt. Mbilu ametoa wito huo leo tarehe 14/05/2023 wakati akihubiri katika Ibada ya Jumapili ya tano baada ya Pasaka (Rogate) iliyofanyika katika Jimbo la Pwani Usharika wa Kana, ambapo amesema  kwa sasa kumekuwa na uwepo wa walimu wanaofundisha mafundisho potofu yanayo wafanya Wakristo kushindwa kuomba kwa usahihi.

Kaimu Mkuu wa Jimbo la Pwani, Mch. Emmanuel Mtoi.

“Nilimkuta mtu mmoja anamuombea mwingine amempigisha magoti anamuombea ili awe tajiri, kuanzia sasa ukitoka hapo nje uokote milioni 50 na   uwe tajiri, maana yake anamuombea mtu mwingine apoteze pesa”.

Askofu Dkt. Mbilu amesema namna bora ya kumuombea mtu ni kumuomba Mungu ampe afya njema ili akafanye kazi zake kwa bidii na kujiongezea kipato ili aweze kuhudumia familia yake kwani hayo ndio maombi yanayotakiwa.

Hata hivyo Askofu Dkt. Mbilu katika Ibada hiyo amemshukuru Mungu kwa kutoa sadaka ya Shukrani kwa makuu Mungu aliyomtendea yeye na uongozi wake, katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake ndani ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

 

“Asanteni wapendwa kwa baraka zenu katika siku yangu ya kuzaliwa lakini siku ya kukumbuka miaka miwili tangu niliposimikwa na kukabidhiwa rasmi wajibu mzito wa kuiongoza Dayosisi yetu ya Kaskazini Mashariki. Mungu atujalie sisi sote nguvu ya kushikamana ili tuitende kazi hii kwa uaminifu mkubwa.