ELCT North Eastern Diocese
Mkuu wa KKKT aanza ziara yake KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki
- Details
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Fredrick Shoo leo tarehe 27/7/2022 ameanza ziara rasmi ya kuitembelea KKKT–Dayosisi ya Kaskazini Mashariki itakayoambatana na kufungua na kuweka mawe ya msingi na kuongea na wana Dayosisi katika maeneo mbalimbali.
Akiwasili katika eneo la Bwiko Usharika Mteule wa Mkumbara Askofu Dkt. Shoo amepokelewa na mwenyeji wake Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu na wana Dayosisi na baadae aliwasili katika Usharika wa Mombo ambapo ameweka jiwe la msingi la Kanisa jipya na kuongoza Ibada ya Shukrani.
Akihubiri neno la Mungu katika Ibada hiyo kutoka kitabu cha Injili ya Mathayo 7:1-5 Mkuu wa Kanisa amekemea tabia za baadhi ya Wakristo kujihesabia haki na kuhukumu wengine hatua inayofifisha vipawa na karama za wengi katika kulijenga Kanisa la Mungu.
Mkuu wa Kanisa amesema kwakuwa hakuna mtu aliyekamilika kabisa hivyo waliowakristo waonyane kwa upendo bila kunyosheana vidole madhaifu ya wengine.
Mbali na hayo Mkuu wa Kanisa ameendesha harambee kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kanisa la Usharika huo wa Mombo na kuchangia kiasi cha shilingi 1,000,000.
Nae Askofu wa KKKT – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Dkt. Msafiri Mbilu amewapongeza wanadayosisi kwa namna walivyojitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Mkuu wa KKKT na kuwasihi kuendelea kujitokeza katika maeneo yote ya Majimbo ambapo Mkuu wa Kanisa atatembelea.
Kesho tarehe 28/07/2022 msafara wa Mkuu wa KKKT utaelekea Bumbuli, ambapo Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo ataendelea na ziara yake katika Jimbo la Kusini kwa kutembelea Usharika wa Bumbuli, Hospitali ya Bumbuli, Chuo cha Utabibu Bumbuli (BUCOHAs) na kisha ataelekea Lutindi ambapo atapata wasaa wa kuwasalimu Washarika wa Lutindi na kutembelea Hospitali ya wagonjwa wa akili Lutindi (Lutindi Mental Hospital).
- Hits: 6954
Matukio katika picha Ibada ya Jumapili.Jimbo la Kaskazini Usharika wa Mbaramo
- Details
MATUKIO KATIKA PICHA: Ibada ya Jumapili iliyokuwa na matukio mbalimbali ikiwemo Ufunguzi wa nyumba ya mwinjilisti pamoja na Ibada ya kipaimara katika Usharika wa Mbaramo ambapo vijana wapatao 85 wamebarikiwa huku mmoja kati yao akibatizwa.Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ndiye aliyeongoza Ibada hiyo.
- Hits: 5643
Askofu Dkt. Mbilu ahimiza elimu juu ya uanzishwaji wa miradi kwa vijana.
- Details
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amesema kuwa elimu kwa vijana juu ya uandaaji na usimamizi wa miradi ni vema sasa ikatolewa katika Dayosisi nzima ili kuwa na vijana wenye uelewa wa kuandaa miradi mbalimbali itakayo wakwamua kiuchumi na kuisaidia jamii.
Askofu Dkt.Mbilu ameyasema hayo leo tarehe 23/07/2022 akiwa katika Usharika wa Muheza kwenye kilele cha mafunzo ya muda mfupi ya uandaaji wa miradi,Tathimini Shirikishi ya Mafunzo (Participatory Learning Appraisal) pamoja na Upangaji wa mradi wenye muelekeo wa matokeo (Result Oriented Project ) yaliyoanza tarehe 11/07/2022 hadi tarehe 23/07/2022 yakijumuisha vijana wapatao 16 wa Usharika huo.
Nimefurahi kwa Usharika,Washarika,Kamati ya miradi kuwawezesha vijana hawa kupata mafunzo haya hasa kwenda vijijini kuona matatizo yalipo katika jamii kuandika miradi kwa wafadhili itakayo wapatia fedha zitakazo isaidia jamii, HILI NI JAMBO ZURI NALA KUPONGEZA. Alisema Askofu Mbilu.
Awali katika Ibada ya Jumuiya iliyo jumuisha jumuiya zote za Usharika huo iliyo ongozwa na Baba Askofu Dkt, Mbilu katika Usharika huo, amemshukuru Mkuu wa Jimbo la Tambarare Mch. Frank Mtangi, Mchungaji wa Usharika wa Muheza Mch. John Ndimbo wakufunzi pamoja na kamati mbalimbali zilizowezesha kufanikisha mafunzo hayo kwa vijana na kutoa wito kwa Majimbo na Sharika zingine kuiga jambo hilo.
- Hits: 5749
Ziara ya Mkuu wa KKKT katika Dayosisi yetu
- Details
Wapendwa wana KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki yahusu ziara rasmi ya kikazi ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Baba Askofu Dkt. Fredrick O. Shoo katika Dayosisi yetu kuanzia tarehe 27/07/2022 hadi tarehe 02/08/2022.
Dhumuni la ziara ya Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo ni kuitembelea KKKT – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, kufungua na kuweka mawe ya msingi. Vilevile Baba Askofu Dkt. Shoo atapata wasaa wa kuongea na wana Dayosisi katika maeneo mbalimbali.
Baba Askofu atawasili katika Dayosisi yetu tarehe 27/07/2022 siku ya jumatano saa 4:00 asubuhi, punde atakapokanyaga ardhi ya Mkoa wa Tanga katika eneo la Bwiko atapokelewa na mwenyeji wake Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu na wana Dayosisi. Ataanza ziara yake siku hiyohiyo ya tarehe 27/07/2022 katika Jimbo la Tambarare kwa kuweka jiwe la msingi la Kanisa jipya katika Usharika wa Mombo muda saa 6:00 mchana.
Aidha mara baada ya uwekwaji wa jiwe la msingi msafara wa Mkuu wa KKKT utaelekea katika Jimbo la Kusini ambapo Baba Askofu Dkt. Shoo ataongea na wana Dayosisi katika Usharika wa Soni yalipo Makao Makuu ya Jimbo hilo majira ya saa 10:00 jioni. Mara baada ya kuongea na wanadayosisi katika Usharika wa Soni siku hiyohiyo msafara utaelekea Kanisa Kuu Lushoto ambapo Mkuu wa KKKT atapokelewa rasmi kwa Ibada maalum saa 11:45 jioni.
Tarehe 28/07/2022 msafara wa Mkuu wa KKKT utaelekea Bumbuli kuanzia saa 2:00 – 6:00 mchana, ambapo Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo ataendelea na ziara yake katika Jimbo la Kusini kwa kutembelea Usharika wa Bumbuli, Hospitali ya Bumbuli na Chuo cha Utabibu Bumbuli (BUCOHAs).
Majira ya saa 7:30 mchana hadi saa 12:00 jioni msafara wa Mkuu wa KKKT utaelekea Lutindi ambapo Baba Askofu atapata wasaa wa kuwasalimu washarika wa Lutindi na kutembelea Hospitali ya wagonjwa wa akili Lutindi (Lutindi Mental Hospital).
Siku ya tarehe 29/07/2022 msafara wa Mkuu wa KKKT muda wa saa 3:00 hadi 6:00 mchana utaelekea katika Jimbo la Tambarare ambapo itafanyika Ibada katika Usharika wa Korogwe na majira ya saa 7:00 mchana msafara utaelekea Jimbo la Pwani.
Tarehe 30/07/2022 saa 3:00 – 6:00 mchana Baba Askofu ataweka jiwe la Msingi wa Kanisa la Makorora na kuongoza Ibada ya kipaimara katika Usharika huo wa Makorora.
Tarehe 31/07/2022 Mkuu wa Kanisa ataongoza Ibada ya jumapili Kanisa Kuu Lushoto kuanzia saa 2:00 – 5:00 asubuhi na majira ya saa 8:00 – 10:00 jioni atatembelea vituo vya Irente Rainbow School, Irente Children’s Home, Irente School for the Blind na Irente Farm.
Tarehe 01/08/2022 saa 4:00 – 5:00 asubuhi msafara wa Mkuu wa Kanisa utaelekea katika Jimbo la Kaskazini ambapo pia kutafanyika Ibada katika Usharika wa Mlalo na majira ya saa 6:30 -8:00 mchana ataelekea katika Shule ya Sekondari Lwandai ambapo Baba Askofu Dkt. Shoo atafungua tena Jengo la Maabara ambalo lilifanyiwa ukarabati na majira ya saa 9:00 – 11:00 jioni msafara wa Mkuu wa Kanisa utaelekea katika Chuo kitarajiwa cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI).
Wito kutoka kwa Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kwa wana KKKT – DKMs, ni kujitokeza kwa wingi kumpokea Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo sehemu zote atakazopita kuanzia Bwiko, Soni, Lushoto, Mlalo, Bumbuli, Lutindi, Tanga, Korogwe na maeneo yote yaliyotajwa atakapokuwa anatembelea, anafungua, anaweka mawe ya msingi na atakapokuwa anaongea nasi.
Mwisho kama ilivyo kawaida na desturi ya wana KKKT-DKMs wakati tunapotembelewa na wageni hasa ugeni mkubwa wa Mkuu wetu wa KKKT, Baba Askofu Dkt. Fredrick O. Shoo, natoa wito tena kwenu kujitokeza kwa wingi tumpokee Mkuu wetu wa Kanisa katika Dayosisi yetu.
- Hits: 6326
Page 47 of 107