Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs), Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amesema ushirikiano kati ya Kanisa, Serikali na wadau wa maendeleo unaendelea kuleta matumaini mapya kwa wananchi kupitia utekelezaji wa miradi ya maji inayolenga kuboresha maisha ya jamii Wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga.Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo leo tarehe 15/05/2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Zephania Sumaye wakati wa kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji iliyokamilika pamoja na inayoendelea kutekelezwa katika kijiji cha Makose-Mtindili, Kata ya Rangwi.Amesema mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 293,000,000 ni hatua muhimu ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama, jambo litakalosaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa maji na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.Kwa mujibu wa Askofu Dkt. Mbilu, mradi huo unatekelezwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa ushirikiano na kampuni ya DENIOS kutoka nchini Ujerumani chini ya Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi Helmut Denning, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza huduma kwa jamii na kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha huduma muhimu kwa wananchi.Naye Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mhe.Zephania Sumaye ameushukuru uongozi wa Dayosisi chini ya Askofu Dkt. Mbilu kwauhusiano mzuri uliopo kati ya Serikali na Kanisa, akieleza kuwa ushirikiano huo umeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Wilaya hiyo. huku akitambua mchango mzuri wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki katika kuihudumia jamii.Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha mradi huo unasimamiwa na kulindwa ili utekelezwe katika viwango vinavyotakiwa, uweze kudumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha wananchi wa sasa pamoja na vizazi vijavyo



