ELCT North Eastern Diocese
Pumzika kwa Amani Mwalimu Wahaki Tawi Vesso
- Details
Ufunuo 14:13 “Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao”.
Picha za matukio mbalimbali ya Ibada ya Mazishi ya Mwalimu Wahaki Tawi Vesso, iliyofanyika leo tarehe 27/05/2023 katika Jimbo la Pwani Usharika wa Kana, Ibada hii iliongozwa na Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, mwili wa Mwalimu Wahaki Tawi Vesso umezikwa katika makaburi yaliyopo Gofu-Goseji-Tanga,
Marehemu Mwalimu Wahaki Tawi Vesso, alizaliwa tarehe 01/05/1942 na kuitwa mbinguni siku ya Alhamisi 24/05/2023 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo akiwa anapatiwa matibabu.
Katika kipindi cha uhai wake aliwahi kuitumikia KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki katika nafasi mbalimbali ikiwemo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu KKKT-DKMS, Mjumbe wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya Bangala, Katibu wa kamati ya Uhusiano ya Usharika kati ya Usharika wa Kana na Berlin Staken Ujerumani pamoja na mwimbaji wa kwaya Kuu ya Usharika wa Kana.
Uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki unaendelea kutoa pole kwa,familia ya marehemu ndugu, jamaa na marafiki popote pale walipo. BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe.
- Hits: 115
Tangazo la nafasi ya kazi Daktari daraja la 2
- Details
TANGAZO LA NAFASI ZA KAZI..
UTANGULIZI
Tarehe 19 Juni 1963, Kanisa la Usambara - Digo na makanisa mengine sita ya Kilutheri yaliungana na kuunda Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT). Leo hii KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs) ni miongoni mwa Dayosisi 27 ndani ya KKKT. Dayosisi inaitwa hivyo kwakuwa inapatikana Kaskazini Mashariki mwa Tanzania katika Mkoa wa Tanga. Kwahiyo KKKT-DKMs ni taasisi ya kidini iliyosajiliwa tarehe 19 Juni 1963 na Makao yake Makuu yapo Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga. Dhamira ya KKKT-DKMs ni kufundisha na kuhubiri neno la Mungu na kutoa huduma nzuri kiroho, kimwili, kiakili, kiuchumi na kijamii kwa watu. Taasisi hii inatoa tangazo la kazi kwa nafasi ifuatayo:
Sifa za waombaji ni kama ifuatavyo;
- DAKTARI DARAJA LA II (NAFASI 2)
Waombaji wawe na Shahada ya Udaktari wa binadamu kutoka Vyuo vikuu/ Vyuo vinavyotambuliwa na Serikali. Waombaji wawe wamemaliza mafunzo ya kazi “internship” ya muda usiopungua mwaka mmoja na kupata usajili kutoka Baraza la Madaktari Tanganyika (Medical Council of Tanganyika)
MASHARTI YA JUMLA YA WAOMBAJI WA KAZI.
- Awe raia wa Tanzania.
- Awe na umri usiopunguza miaka 18 na usiozidi miaka 45.
- Awe na vyeti kamili vya mafunzo ya fani aliyosomea (Cheti cha Kidato Cha Nne, Sita, Taaluma na usajili kamili (Full Registration) au leseni hai ya kufanya kazi ya taaluma husika.
- Mwombaji aliyewahi kuajiriwa serikalini na kupata cheki namba, atatakiwa kuzingatia utaratibu wa kuomba kibali cha kurejea katika utumishi wa umma na kuendelea kutumia cheki namba baada ya kuacha kazi kama ilivyobainishwa kwenye waraka na. CCB.228/271/01 wa tarehe 7 Agosti 2012.
- Mwombaji awe na sifa na weledi kwa mujibu wa waraka wa maendeleo ya Utumishi Namba. 1 wa mwaka 2009 kuhusu kada zilizo chini ya Wizara ya Afya kama ilivyoainishwa hapo juu.
- Waombaji wenye elemavu watapewa kipaumbele katika ajira hii kwa kuzingatia sheria ya watu wenye ulemavu Na. 1 ya mwaka 2010.
MAOMBI YOTE YAAMBATANISHWE NA,
- Nakala ya cheti cha kuzaliwa.
- Nakala ya cheti cha kidato cha nne au/ na cha sita au stashahada kulingana na kada ya mwombaji. Kwa aliyesoma nje ya nchi au mitaala ya nje ya nchi waambatanishe cheti cha ithibati kutoka baraza la mitihani Tanzania (NECTA).
- Nakala ya vyeti vya Taaluma na Transcript, Aidha waliosoma vyuo vya nje ya nchi, waambatishe cheti cha Ithibati kutoka TCU.
- Wasifu (CV).
- Nakala ya cheti cha Usajili na Leseni hai ya taaluma husika (Full Registration & Valid Licence).
- Nakala ya cheti cha Mafunzo kwa vitendo (Internship).
- Picha ndogo (passport size) moja ya hivi karibuni.
- Nakala ya kitambulisho cha uraia (NIDA/ Namba ya NIDA).
- Iwapo majina yako yanatofautiana katika vyeti vyako Pamoja na cheti cha kuzaliwa na NIDA hakikisha unawasilisha kiapo cha majina (Deed Pool) kutoka kwa Msajili wa viapo na kusajiliwa na Msajili wa hati, wizara ya Ardhi na maendeleo ya makazi.
NAMNA YA KUTUMA MAOMBI.
Maombi yote yatumwe ndani ya wiki mbili tangu tarehe ya kutoka kwa Tangazo hili (Mwisho wa kutuma maombi ni Tarehe: 06/06/2023). Maombi yote yatumwe kwa Ofisi ya Katibu Mkuu-KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki S.L.P 10 LUSHOTO Au: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
- Hits: 437
KOTETI YAANZA UDAHILI KWA MWAKA WA MASOMO 2023-2024 KOZI YA FAMASIA (Pharmacy).
- Details
Uongozi wa Taasisi ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto-Tanga, yenye usajili namba KOTETI/HAS/249 unapenda kuwatangazia nafasi za masomo kwa muhula mpya 2023/2024 kwa kozi ya famasia yaani Diploma in Pharmaceutical science kwa miaka mitatu (3).
SIFA ZA KUJIUNGA. muombaji awe na kiwango cha alama kuanzia "D" nne (4) na kuendelea katika masomo ya Chemistry na Biology na masomo mengine yoyote mawili isipokuwa ya dini. Ada ni shilingi 1,400,000/= na italipwa kwa awamu. Hosteli nzuri na huduma ya chakula vinapatikana kwa bei nafuu kabisa. Ili kupata fomu za kujiunga ingia kwenye tovuti ya chuo www.koteti.ac.tz au tembelea ofisi za chuo kwa maelezo Zaidi au tuma barua pepe kwa This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. au piga simu namba
0712 811 420 au 0747 067 565 au 0784 370 200
Wote mnakaribishwa
- Hits: 419
Askofu Dkt. Mbilu azindua Ushirika wa Wanafunzi wa Kikristo wa Vyuo vikuu na vya kati (USCF).
- Details
HABARI PICHA: Picha za matukio mbalimbali ya uzinduzi wa Ushirika wa Wanafunzi wa Kikristo wa Vyuo vikuu na vya kati (USCF) uliofanyika leo tarehe 14/05/2023 katika ukumbi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Tanga.Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ambaye pia ni Katibu wa CCT Mkoa wa Tanga alimumuingiza kazini Mch. Rogers Chamani wa Kanisa Anglican kuwa Mratibu wa USCF Mkoa wa Tanga.
- Hits: 812
Page 1 of 85