Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu alizaliwa tarehe 9 Mei, 1968 katika kijiji cha Kwang’wenda, Soni, Wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga.
Askofu Dkt. Mbilu. alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Msingi Kwang’wenda, Lushoto. Mwaka 1985-1988 alipata elimu ya sekondari katika shule ya sekondari Namfua iliyopo Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro. Alipata elimu ya Theologia katika Chuo cha Theologia, Makumira mwaka 1990- 1994 na kumaliza masomo ya General Certificate in Theology.
Mwaka 1997 alijiunga na masomo ya shahada ya Theolojia Chuo kikuu cha Makumira na kuhitimu mwaka 2000. Alipata shahada ya uzamili ya Theolojia mwaka 2000-2002 huko Norway, katika chuo cha Stavanger School of Mission and Theology.Mwaka 2006-2012 alijiunga na chuo kikuu cha Kirchliche Hochschule Wuppertal cha nchini Ujerumani ambapo alitunukiwa shahada ya uzamivu katika Theolojia.
Mwaka 1996 alisoma Kozi Maalum ya muziki katika chuo cha Day Star University Nairobi Kenya (Church Music and African Traditional Music) amewahi pia kuwa Mwalimu katika Chuo cha Biblia Vuga 1994-1997 na pia amewahi kuwa Mchungaji Kiongozi Usharika wa Mombo, mwaka 1997-1999 na Usharika wa Korogwe 2003.Aliwahi pia kuwa Mkuu wa Jimbo la Kaskazini na Mchungaji wa Usharika wa Mlalo kuanzia mwaka 2004 hadi 2006, na mwaka 2012 alikuwa Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kange.
Askofu Dkt. Mbilu amewahi kuwa Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira 2012- 2015. Pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa kituo cha Tanga cha Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastiani Kolowa, (SEKOMU) mwaka 2015-2016.
Vilevile alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho kati ya mwaka 2016 hadi 2018 na mhadhiri chuoni hapo katika masomo ya Agano Jipya na Lugha za Biblia (Kigiriki).Hadi siku anachaguliwa kuwa Askofu Mteule wa KKKT-DKMs, Askofu Dkt. Mbilu alikuwa Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo kikuu cha Silliman kilichoko nchini Philippines, akifundisha masomo ya Agano Jipya na Lugha za Biblia (Greek na Hebrew).
NDOA
Alifunga ndoa na Dkt.Mary Joseph Jali Desemba 9, 1995 na wamejaliwa kupata watoto watatu, Dkt.Sarah Mbilu, Mhandisi Joseph Mbilu, na Jackson Mbilu.



