.Askofu wa KKKT–Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs), Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amempokea na kumpongeza Mch. Dkt. Nuru Mwakapusya baada ya kuwasili na kuripoti rasmi katika Ofisi za Makao Makuu ya Dayosisi zilizopo Lushoto, Mkoa wa Tanga, kufuatia kukamilisha masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Silliman, nchini Ufilipino.
Mch. Dkt. Nuru amehitimu Shahada ya Uzamivu ya Theolojia yaani (Doctor of Theology) akiwa amebobea katika Maadili ya Kikristo (Christian Ethics). Alianza masomo yake mwaka 2022 na kuhitimu mwaka 2026.
Askofu Dkt. Mbilu mara baada ya kumpokea na kufanya mazungumzo na Mch. Dkt. Nuru amempongeza kwa mafanikio hayo makubwa ya kitaaluma, akieleza kuwa elimu aliyoipata ni rasilimali muhimu kwa Dayosisi, Kanisa la Mungu na jamii kwa ujumla.
Aidha, alimtakia baraka na hekima katika kuendeleza kuitenda huduma aliyoitiwa.Mch. Dkt. Nuru alieleza kuwa anamshukuru Mungu ambaye amemuwezesha hadi kufikia hatua hiyo huku akiwashukuru UEM (United Evangelical Mission) kwa kufadhili wa masomo yake kwa ukamilifu wake kwa kipindi chote cha masomo.
Pia aliishukuru KKKT–Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa ushirikiano, msaada na maombi yaliyomwezesha kufanikisha safari yake ya kitaaluma.Katika utafiti wake wa shahada ya uzamivu uliokuwa na kichwa cha habari, "An Ethical Analysis of Church's Response to the Trafficking of Women in Tanga, Tanzania," Mch. Dkt. Nuru alichambua kwa kina mwitikio wa Kanisa katika kukabiliana na tatizo la usafirishaji haramu wa wanawake kwa mtazamo wa maadili ya Kikristo.
Alieleza kuwa matokeo ya utafiti huo yataisaidia Kanisa na jamii kushirikiana katika kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya biashara haramu ya binadamu, kuhimiza ulinzi wa utu na haki za binadamu pamoja na kuimarisha huduma kwa waathirika. Aidha, utafiti huo unahamasisha ushirikiano kati ya Kanisa, Serikali na wadau mbalimbali katika kuzuia biashara haramu ya binadamu na kujenga jamii yenye usalama, haki na heshima kwa wanawake na wasichana.
Mafanikio haya ni ushuhuda wa uwekezaji wa Kanisa na wadau wake katika kuimarisha elimu ya watumishi wake, ili waendelee kutoa huduma yenye ubora na mchango chanya kwa Kanisa na taifa kwa ujumla


