Contact Info

P.O Box 10 Lushoto Tanga Tanzania

+255

headoffice@elctned.org

ELCTNED

Latest Posts

Salamu za Pongezi kwa Dkt. Lemmi Tamilwai Baruti

Uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, chini ya Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, unatoa salamu za pongezi kwa Mchungaji Dkt. Lemmi Tamilwai Baruti kwa mafanikio ya kukamilisha masomo ya Shahada ya Uzamivu (Doctor of Philosophy in Theology Systematic Theology) katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (University of South Africa – UNISA), kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2026.

Mafanikio haya ni hatua muhimu katika safari ya huduma ya kichungaji na kitaaluma ya Mch. Dkt. Lemmi Baruti, pamoja na kuwa mchango mkubwa katika kuimarisha tafakari ya kitheolojia kuhusu nafasi ya Kanisa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.

Katika utafiti wake Mch. Dkt. Lemmi Baruti amechunguza namna Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania linavyoweza kuchangia katika utekelezaji wa sera za viwanda nchini Tanzania kwa kutumia misingi ya theolojia ya ukombozi wa kisiasa na kiuchumi.

Utafiti huo unalenga kuchunguza nafasi ya Kanisa katika kuhamasisha maendeleo ya viwanda, kupunguza umaskini, kutetea haki za kiuchumi na kijamii, pamoja na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Kwa kuangazia masuala haya, utafiti unaweka msingi wa kutafakari namna mafundisho ya Kikristo na misingi ya kitheolojia inavyoweza kuhusishwa na changamoto halisi za kiuchumi na kijamii zinazolikabili taifa, hususani katika juhudi za kujenga uchumi unaozingatia haki, usawa na utu wa binadamu.

Utafiti huu unatoa mchango muhimu katika eneo la theolojia ya kimfumo, haki za binadamu, haki ya kijamii na heshima ya utu wa binadamu.Aidha, mfumo unaopendekezwa katika utafiti huo unatoa mtazamo wa namna maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanavyoweza kuimarishwa kupitia ushirikiano wenye tija kati ya Kanisa na Serikali.

Ushirikiano huo unalenga kuchochea mabadiliko yanayoweza kuleta manufaa kwa wananchi, hasa katika masuala ya uzalishaji, kupunguza umaskini na kuboresha ustawi wa jamii.Utafiti huu pia unaibua nafasi ya Kanisa katika kushiriki mijadala ya kitaifa kuhusu sera za maendeleo, kwa kuzingatia misingi ya imani, haki, uwajibikaji na huduma kwa jamii.

KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki inampongeza Mch. Dkt. Lemmi Tamilwai Baruti kwa juhudi, uvumilivu na kujituma kwake katika kukamilisha masomo haya ya juu.Dayosisi ina matumaini kwamba elimu na maarifa aliyoyapata yatakuwa chachu ya kuimarisha huduma ya Kanisa, kukuza tafiti za kitheolojia na kuchangia mijadala na jitihada za maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.

Mafanikio haya ni ushuhuda wa umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya watumishi wa Kanisa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuchangia maendeleo ya Kanisa na taifa kwa ujumla.Hongera sana Mch. Dkt. Lemmi Tamilwai Baruti kwa mafanikio haya makubwa.

Uongozi wa Dayosisi pia unatoa shukrani za dhati kwa United Evangelical Mission (UEM) kwa ushirikiano na ufadhili wa masomo uliowezesha kukamilika kwa masomo hayo.

Tufuatilie kupitia:
Facebook Account: North Eastern Diocese
Facebook Page: ELCT – North Eastern Diocese
YouTube: KKKT DKMS Online TV
Website: www.elctned.org