Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameongoza harambee na kufanikisha kuchangisha shilingi bilioni 1.06 kwa ajili ya kuchangia kazi za maendeleo na maboresho ya vituo vya huduma na diakonia vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs).
Harambee hiyo imefanyika leo, Jumatatu, Oktoba 5, 2026, katika viwanja vya Tanga Beach Resort, Jijini Tanga, ambapo kati ya fedha zilizopatikana, shilingi milioni 617.06 ni fedha taslimu, huku shilingi milioni 442 zikiwa ni ahadi.
Akizungumza katika harambee hiyo akiwa mgeni rasmi, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu amewataka Watanzania kushiriki kugharamia huduma kwa watu wenye ulemavu na watoto walio katika mazingira magumu, akisema kupungua kwa misaada kutoka kwa wahisani wa nje hakupaswi kuathiri upatikanaji wa huduma kwa makundi hayo.
Waziri Mkuu amelipongeza Kanisa kwa kutoa huduma za elimu, afya na malezi bora, akisisitiza kuwa watoto hawapaswi kukosa elimu kutokana na ulemavu. Pia amewataka viongozi wa halmashauri kuwasaidia watu wenye ulemavu wasioweza kujitegemea, badala ya kuwapa barua za kuzunguka kuomba michango.
Awali, Askofu wa KKKT-DKMs, Dkt. Msafiri Mbilu, alimweleza Waziri Mkuu kuwa huduma kwa watu wenye ulemavu na watoto walio katika mazingira magumu ni sehemu ya mchango wa Kanisa kwa jamii na Serikali katika kuhakikisha wananchi, bila kujali hali zao, wanapata fursa ya kuishi kwa utu na kushiriki katika maendeleo.
KKKT-DKMs, yenye makao Makuu Wilayani Lushoto, inaendesha vituo mbalimbali vya huduma na Diakonia, vikiwemo Lutindi Mental Hospital, Bumbuli Lutheran Hospital, Kilindi Hospital, Kituo cha Watoto Yatima Irente, Shule ya Wasioona Irente na Irente Rainbow School inayohudumia watoto wenye ulemavu wa akili na usonji, pamoja na shule na vyuo mbalimbali.
Baadhi ya vituo hivyo vina historia ya zaidi ya karne moja.Hata hivyo, Askofu Dkt. Mbilu amesema vituo hivyo vinakabiliwa na changamoto zikiwemo uchakavu wa miundombinu, upungufu wa vifaa tiba na vifaa vingine muhimu vya huduma, pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma, hususan katika afya ya akili, ulemavu na huduma kwa watoto walio katika mazingira magumu.



