Askofu wa KKKT–Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ameongoza kikao cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi kilichofanyika Utondolo, Lushoto, tarehe 19 Novemba 2026.
Katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine, taarifa kutoka Kurugenzi za Mission na Uinjilisti, Fedha na Utawala, Uchumi, Mipango na Maendeleo, pamoja na Huduma za Jamii, zimewasilishwa kwa wajumbe.
Awali, Askofu Dkt. Msafiri Mbilu aliwatambulisha kwa wajumbe wa Kikao hiki, Mch. Dkt. Nuru Mwakapusya na Mch. Dkt. Lemmi Tamilwai Baruti, ambao wamehitimu masomo yao ya Shahada za Uzamivu hivi karibuni.Mch. Dkt. Nuru Mwakapusya amehitimu Shahada ya Uzamivu ya Theolojia (Doctor of Theology), akibobea katika Maadili ya Kikristo (Christian Ethics).
Naye Mch. Dkt. Lemmi Tamilwai Baruti amehitimu Shahada ya Uzamivu ya Falsafa katika Theolojia (Doctor of Philosophy in Systematic Theology) katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (University of South Africa – UNISA). Utafiti wake unachunguza nafasi ya Kanisa katika kuhamasisha maendeleo ya viwanda, kupunguza umaskini, kutetea haki za kiuchumi na kijamii, pamoja na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Aidha, wajumbe wa kikao hicho walipata fursa ya kuliona gari ambalo ununuzi wake ulitokana na maamuzi yao katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi kilichofanyika tarehe 23–24 Aprili 2026, Utondolo, Lushoto.
Kupitia Agenda Na. 5 iliyohusu mambo kutoka Kamati ya Utendaji, kikao hicho kiliazimia kununuliwa kwa gari hilo kwa ajili ya Jimbo la Magharibi.



