Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt. Msafiri Joseph. Mbilu ambaye yupo nchini Ujerumani kwa ziara ya kikazi, leo tarehe 27/05/2026 akiwa kwenye mwendelezo wa ziara yake ameshiriki hafla ya kurejesha ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Hannover (Leibniz University Hannover) - Kitivo cha Elimu Maalumu na KKKT-DKMs.
Hafla hiyo iliambatana na uzinduzi wa mradi mpya wa kuimarisha Afya na makuzi ya watoto wadogo, hususani watoto yatima na walio kwenye mazingira hatarishi (A Network of Knowledge: Fostering Early Childhood Health in Low-resource Communities – Prevention and Education through a Community-Based Network in Rural Tanzania).
Lengo la mradi huu ni kuwajengea maarifa ya kuwatunza watoto yatima na walioko kwenye mazingira hatarishi wafanyakazi wa Kituo cha Watoto Yatima Irente na Shule ya watoto wenye ulemavu wa akili na usonji Irente (Irente Rainbow School), pamoja na jamii kwa ujumla ili kuepusha ulemavu na changamoto mbalimbali zinazoweza kuwakumba watoto walio kwenye makundi haya.
Mradi huu utafanyika kwenye majimbo yote 5 ya Dayosisi ambayo yapo katika Mkoa wote wa Tanga.Pamoja na mafunzo yatakayotolewa katika makundi hayo, mradi huu una lengo la kuimarisha kozi mpya ya Elimu ya awali na makuzi (Early Childhood Education and Development) itakayoanzishwa katika Taasisi ya Elimu ya KOTETI katika mwaka wa masomo 2026/2027.
Mradi huu unaofadhiliwa na Wizara ya Mambo ya Jamii, Afya na Usawa Jimbo la Lower Saxony Ujerumani ni wa miaka mitatu na utafanyika kwa awamu tatu na unatarajiwa kugharimu kiasi cha Euro 47,000 sawa na Tsh 126,900,000 kwa awamu ya kwanza.



