
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs) Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amefanya ziara ya kikazi katika Shule ya Sekondari ya Lwandai inayomilikiwa na KKKT-DKMs iliyopo Lushoto Mlalo leo tarehe 13/08/2024 ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu wa Ofisi ya Askofu kutembelea vituo vinavyomilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Askofu Dkt. Mbilu ameupongeza uongozi wa shule ya Lwandai,wanajumuiya ya Lwandai pamoja na wanafunzi kwa juhudi na mafanikio makubwa wanayoyaonyesha kwa ufaulu mzuri na amewaasa wanafunzi wasome kwa bidii na zaidi kwa wale ambao wapo madarasa ya mitihani ilikufikia lengo la kuondoa divisheni 3.

Sambamba na hayo, Askofu Dkt. Mbilu amefurahishwa na maonyesho kwa vitendo ya maabara ya Fizikia na Kemia yaliyofanywa na wanafunzi wa kidato cha kwanza, cha pili na cha nne,amejionea fahari ya kuwa na maabara bora na ya kisasa kwa jinsi wanafunzi walivyoonyesha ustadi katika maonyesho hayo.

Wanafunzi waliweza kutenganisha udongo kwenye maji na kupata maji masafi,walitengeneza hewa ya Oksjeni na kutengeneza mfumo wa breki za gari (Hydraulic Brake). Ni maonyesho yalionyesha Lwandai kuwa Shule bora na nzuri kwa mwanafunzi kupata kilichobora kwasababu wana walimu wenye ujuzi wa hali ya juu ya ufundishaji na pia kuwajengea Wanafunzi uwezo wa kujiamini katika masomo.

Askofu Dkt. Mbilu alitembelea miradi mbalimbali inayomilikiwa na Shule hiyo ambapo kuna mradi wa ufugaji wa nyuki, nguruwe, samaki, sungura na shamba la kabichi na ngano huku akitoa wito kwa uongozi kuendelea kubuni miradi mingine mingi na kusisitiza ufugaji wa kisasa wa samaki. Katika ziara hii Askofu Dkt. Mbilu aliambatana na Mkuu wa Jimbo la Kaskazini Mch. Anderson Kipande pamoja na Mkurugenzi wa Huduma za Jamii wa KKKT-DKMs Mwl. Afizai Vuliva.

