Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt Msafiri Joseph Mbilu,amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha Watanzania kuendelea kujitokeza katika zoezi la kujiandikisha katika daftari la wapigakura huku akiwataka  Watanzia wote kutumia  muda uliobaki kuendelea kujitokeza katika Vituo mbalimbali vya kujiandikisha  kwa kuwa ni wajibu kushiriki katika kuchagua viongozi watakaoweza kuwasaidia wananchi.

Askofu Dkt Mbilu ametoa witu huo leo tarehe 14/10/2024 mara baada ya kujiandikisha kwenye daftari la Wapigakura kwaajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Kituo cha kujiandikisha cha Uwalu Wilayani Lushoto Mkoani Tanga na kuwasihi Watanzania wote kuendelea kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha ili kutimiza haki yao ya kimsingi ya kikatiba ya yakupiga kura wakati utakapofika.

Sambamba na hayo ikiwa leo pia ni kumbukizi ya miaka 25 ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Askofu Dkt.Mbilu ameongeza kwa kusema kuwa katika kipindi hiki cha uchaguzi ni vema viongozi wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kujitenga na vitendo vya rushwa kwani kwakufanya hivyo watakuwa wamemuenzi Baba wa Taifa ambaye alikimea waziwazi vitendo vya rushwa kwani mtu anayetumia rushwa kupata uongozi huyo hafai kwa sababu anafanya hivyo kwa manufaa binafsi badala ya wananchi wanaompa kura.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Zephania Steven Sumaye amesema kuwa uelewa kwa wananchi juu ya kujiandikisha iliwapate sifa ya kupiga kura wakati utakapofika umeendelea kuwa mkubwa Wilayani Lushoto huku akiwataka wananchi kuendelea kujitokeza huku akiwashukuru viongozi wa Dini ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha waumini na wananchi.Mkuu huyo wa Wilaya kipekee amemshukuru Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluthuri Tanzania Dayosisi ya Kaskazi Mashariki Dkt.Msafiri Joseph Mbilu, kujitokeza kujiandisha na kuwahimiza watanzania katika zoezi zima la kujiandikisha.