
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs), Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ambaye pia ni msimamizi Mkuu wa mali za Dayosisi amesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Chuo cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) kinacho milikiwa na KKKT-DKMs na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), makubaliano yanayolenga kuboresha na kukuza taaluma na tafiti katika vyuo hivyo.
Makubaliano hayo yamefanyika leo 13/02/2025 katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Chuo cha SUA kilichopo Morogoro ambapo Askofu Dkt. Mbilu amesema ushirikiano huo utaimarisha Chuo cha KOTETI kwa kutoa fursa za mafunzo ya kozi mbalimbali na kufanyika kwa tafiti za kisasa katika Sekta ya Kilimo cha mbogamboga,Misitu,Ufugaji wa ngombe na samaki jambo ambalo litachochea pia maendeleo kwa jamii ya Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla.

Askofu Dkt.Mbilu amesema kutokana na Chuo cha SUA kuwa na wataalamu wabobevu katika masuala ya kilimo na Misitu ushirikiano huo utasaidia kuboresha na kuendeleza maeneo ya misitu na mashamba yanayo milikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambayo ni Raslimali kubwa kwa Dayosisi .
Kwa upande wake makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda akizungumza katika utiaji saini wa makubaliano hayo , ameupongeza uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa uamuzi wa kukichagua Chuo hicho katika ushirikiano huo na kuahidi kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia malengo ya makubaliano hayo.
Mawanda ya ushirikiano huo yamejikita hususani katika kuendesha kozi mbalimbali kwa pamoja,kufanya tafiti mbalimbali, kuandika maandiko yanayotokana na tafiti ,kuendesha shughuli za kilimo cha mafunzo (Shamba darasa) ambayo yatahusisha wanafunzi na jamii kwa ujumla, pamoja na shughuli za ki maabara.

Tufuatilie kwenye mitandao yetu ya kijamii
INSTAGRAM - / elctned
FACEBOOK ACCOUNT North Eastern Diocese
FACEBOOK PAGE - ELCT-North Eastern Diocese
YOUTUBE - / KKKT DKMS Online TV
WEBSITE : https://elctned.org/
KWA MAONI NA USHAURI:
Simu : +255 743 399 798