Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs), Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Halmashauri ya Katiba ya KKKT, juu ya zoezi linaloendelea la kuchukuwa maoni juu ya Katiba Mpya ya KKKT na kusema kuwa anaamini Katika Mpya ya KKKT, itakuwa jumuishi na italeta umoja wa kweli katika Kanisa.
 
Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo leo tarehe 22/04/2025 mara baada ya Kikao cha Halmashauri Kuu Maalumu ya KKKT-DKMs iliyoitishwa kwaajili ya kutoa maoni juu ya Katiba Mpya ya KKKT. Kikao hicho kimefanyika Katika ukumbi wa Mikutano Utondolo Lushoto ambapo kamati ya Halmashauri ya Katiba ya KKKT ilipokea maoni hayo kutoka kwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.
 
Kamati hii inaongozwa na Mwenyekiti wake Baba Askofu Charles Mjema wa KKKT-Dayosisi ya Pare akishirikiana na Askofu Dkt. Godson Abel Mollel wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Kati (Arusha), Askofu Dkt. Syprian Yohana Hilinti wa Dayosisi ya Kati (Singida), Bw. Simon Daffi ambaye anamuwakilisha Katibu Mkuu wa KKKT kwenye mzunguko huu pamoja na wajumbe wengine ambao pia walipata nafasi ya kutembelea Makao Makuu ya KKKT-DKMs na kusaini kitabu cha wageni.
 
Pamoja na hayo Bw. Ombeni Lance, ambaye ni makamu mwenyekiti kamati ya KKKT Marathon, alipata nafasi ya kutoka maelezo katika kikao hicho juu ya KKKT Marathoni inayotazamiwa kufanyika tarehe 21/06/2025 Jijini Arusha ambapo alieleza kuwa KKKT Marathon ni mbio maalum zilizoandaliwa kwa ajili ya wana KKKT wote katika kuleta mshikamano na kuimarisha umoja wa Kanisa.
Marathoni hii ambayo itajumuisha mbio tano yaani; kilomita 2.5, 5,10, 21 na 42.9 kauli mbiu yake ni; “Kimbia kwa Moyo, Saidia kwa Upendo.
 
TAARIFA ZAIDI JUU YA MBIO HIZI BONYEZA KIUNGANISHI (LINK) HIKI HAPA CHINI.