
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch. Dkt Msafiri Joseph Mbilu, leo tarehe 04/12/2021 ameongoza Ibada ya kipaimara ambapo vijana wapatao 109 walibarikiwa na wanne kati yao walibatizwa katika Ibada iliyofanyika Usharika wa Mtonga.


Askofu Dkt.Msafiri Mbilu amewasihi vijana walio pokea Kipaimara kuendelea kuwa na moyo wa kumtumikia Mungu na wasidanganywe na Dunia iliyojaa mafundisho potofu ya neno la Mungu, bali waendelee kusimama katika mafundisho sahihi ya neno la Mungu na kumtumikia kwa vipawa alivyo wajalia.

Mbali nahayo Askofu Dkt Mbilu amekazia ujumbe wake wa kuwataka watendaji ndani ya Dayosisi kujikita katika utumishi uliotukuka na kujiepusha na matumizi yasiyo faa ya mali na fedha za Dayosisi.

Awali wakati akitoa salamu za Ofisi Kuu ya Dayosisi Kaimu Katibu Mkuu Mch. Godfrey T. Walalaze amewashukuru washarika wa Usharika wa Mtonga kwa namna wanavyo jitoa katika kuifanya kazi ya Mungu, pia amewaeleza washarika wa Usharika wa Mtonga na kipekee Jimbo la Tambarare kutumia fursa ya ardhi waliyonayo kuwekeza kwenye kilimo cha zao la Mkonge.


Liturgia katika Ibada hiyo iliongozwa na Mkuu wa jimbo la Tambarare Mch. Frank Richard Mntangi, na Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu alihubiri neno la Mungu. Ibada ilihudhuriwa na Wachungaji, Wainjilisti, Mashemasi, Kwaya, Washarika pamoja na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Usharika wa Mtonga.






