Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Kalisti Lazaro ametoa wito kwa kamati ya amani ya viongozi wa Dini mbalimbali (Interfaith) kuendelea kuwa mabalozi wa kulinda amani na upendo kwa kuhubiri katika nyumba zao za Ibada ili kuzuia matukio ya ukatili pamoja na mauwaji ambayo yamekuwa yakishamiri maeneo mbalimba Nchini sambamba na kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa sensa ambayo inatarajiwa kufanyika mwezi wa nane mwaka huu.

 

Ametoa wito huo wakati akizungumza na viongozi hao katika semina iliyofanyika leo tarehe 10/02/2022 katika ukumbi wa Utondolo wilayani Lushoto na kusema kuwa viongozi wa Dini wanayo nafasi kubwa ya kutoa elimu kwa waumini wao pamoja na kumuomba Mungu ili roho za ukatili Lushoto pamoja na taifa kwa ujumla ziweze kutoweka.

Sambamba na hilo amewataka viongozi hao kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuiletea Nchi maendeleo kwakutoa fedha ambazo zimekuwa ni chachu ya maendeleo kwa taifa.

 

Kwa upande wake katibu wa kamati ya Interfaith wilaya ya Lushoto Mohamed Said Baruti pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Shekh Mohamed Hamisi pamoja na Mch Leonard Mweri wamesema elimu waliyoipata katika semina hiyo imewajengea upeo mpana wa kwenda kutoa elimu sahihi kwa jamii ikiwemo maswala ya sensa,amani pamoja na namna ya kujikinga na ugonjwa wa uviko 19.

 

Awali mwenyekiti wa kamati hiyo ya amani (W) Lushoto Mch. Michael Mlondakweli Kanju akimkaribisha mkuu wa Wilaya ya Lushoto amemhakikishia kuwa kamati hiyo itaendelea kutoa Ushirikiano kwa serikali na kushiriki  katika kazi mbalimbali ili kuendelea kuiletea maendelea Wilaya ya Lushoto na Nchi kwa ujumla, Mch Michael Kanju ambaye pia ni mzaidizi wa Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki alichaguliwa mnamo tarehe 01/02/2022 kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo.