
Mungu aliuumba ulimwengu mzuri na kutupa jukumu la kuutunza bila kujali dini yoyote kwani yakitokea madhara yanayo sababishwa na uharibifu wa mazingira huadhiri jamii nzima hayo yamesemwa na Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 49 wa kujenga mahusiano mema kati ya Dini za Kiyahudi, Kikristo na Kiislamu( JCM), uliofunguliwa leo tarehe 22/02/2022 kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa SEKOMU.(JCM) ilianzishwa mnamo mwaka 1960, washiriki wakiwa ni Wakristo,Wayahudi na Waislam,lengo likiwa ni kuiasa jamii kutunza mazingira na kupambanua changamoto ya mabadiliko ya tabia ya Nchi.

Naye mgeni rasmi katika ufunguzi huo Mhe Kalisti Lazaro Mkuu wa Wilaya ya Lushoto amesisitiza kuwa umefika wakati sasa dini itumike kupaza sauti katika kueleza kwa kina juu ya athari na umuhimu wa kutunza mazingira kwa vile jitihada za kutafuta maisha zimepunguza imani za kidini na kupuuza mafundisho,kutojali uhalisia wa utu.

Ameongeze kuwa “kila mtu ni mchunga na kila mchunga ataulizwa juu ya kile alichokichunga”. umefika wakati wa kutumia ndimi zetu, vitabu vyetu na elimu zetu tulizonazo, katika kuwaeleza kwa kina wafuasi wetu kuhusu athari hasi za kimazingira ili kuilinda Dunia na viumbe vilivyomo ndani yake.

Aidha ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kutimiza matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 ambayo imeweka wazi misingi ya jumla katika suala zima la uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na haki ya kuwa na mazingira safi, salama na ya kiafya, wajibu wa kulinda mazingira, misingi ya usimamizi wa mazingira pamoja na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira.

Hivi karibuni tu tarehe 12 Februari, 2022 tulishuhudia tukio muhimu ambapo Sera ya Taifa ya Mazingira 2021 ilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango. Sera hiyo pamoja na mambo mengine inaelekeza kwa kina namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa vyanzo vya maji, uchafuzi wa hali ya hewa na mikakati ya kukabiliana na upotevu wa wanyama pori na viumbe hai vinavyoishi ardhini na majini.

UEM: United Evangelical Mission ni umoja wa kiinjili wa kimisheni kilichoanzishwa miaka 25 iliyopita na wamisionari kutoka Ujerumani wa Rhenish na Betheli ambao walifika Africa, na Asia kwa ajili ya kuanzisha shughuli za Dini. Katika Africa walifika katika nchi 7 ambazo ni Tanzania, DR Congo, Africa ya Kusini, Botswana, Cameroon, Namibia na Rwanda kukiwa na madhehebu 15. Katika Tanzania inawakilishwa na Makanisa 4 ya KKKT ambayo ni KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani pamoja na KKKT Dayosisi ya Karagwe.

Aidha Chama hiki ambacho ndicho kinacho ratibisha mkutano huo kinashughulika katika nguzo tano ambazo ni Uhusiano/ Undugu, Diakonia, Uinjilishaji, Utetezi pamoja na Maendeleo.


