Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amezindua rasmi shughuli za uchimbaji wa madini Vuga Kihitu yaliyopo katika shule ya sekondari ya Bangala na kuwataka wachimbaji kufuata na kuheshimu sheria zilizowekwa ili kulinda na kudumisha amani.

Akimuwakilisha Askofu Dkt. Mbilu katika uzinduzi huo msaidizi wa Askofu Mch. Michael Kanju amesema kuwa uchimbaji huo unafanyika kwa mujibu wa sheria za Nchi hivyo kuwataka wachimbaji hao kutokuvunja sheria sambamba na kuwaasa kutambua eneo hilo ni sehemu ya kuwainua kiuchumi.

Nae Mch John Ndimbo kutoka Ofisi kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki amefanya maombi maalumu ili kuliombea eneo hilo huku akiwaasa wachimbaji hao kumshirikisha Mungu na kuacha kutumia njia nyingine ikiwemo za ushirikiana ambazo zitakuwa ni chukizo kwa Mungu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uchumi Mipango na Maendeleo David Chanyengea amesema kuwa wameweka utaratibu maalumu kwa uchimbaji wa madini hayo na tayari mnunuzi wa madini hayo ameshapatikana.

Nao baadhi ya wachimbaji katika mgodi huo akiwemo Alphan Maduda pamoja na Yusuph Ally wamewashukuru viongozi wa Dayosisi kuruhusu eneo hilo kuchimbwa huku wakiahidi kufuata sheria na maagizo yaliyotelewa na viongozi hao.