
JUMAPILI ya Mei 9 mwaka 2021, shughuli za mji wa Lushoto na viunga vyake zilisimama kwa muda huku macho na masikio yote yakiwa kwenye tukio la Ibada ya kuingizwa kazini kwa Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu kuwa Askofu wa awamu ya tano wa KKKT-DKMs.
Leo tarehe 09/05/2022 Askofu Dkt Msafiri Mbilu anafikisha mwaka mmoja tangu kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.Askofu Dkt Mbilu anaendelea kuwakumbusha watumishi kusimama imara ili kuhubiri neno la Mungu kwa usahihi na kusimamia mafundisho sahihi ya neno la Mungu na kuondokana na mafundisho potofu yanayopelekea kujenga roho ya uvivu na wasiwasi katika jamii.

Mhadhiri huyo mwandamizi wa chuo Kikuu cha Silliman cha Nchini Ufilipino, aliingizwa kazini katika Ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Lushoto na kisha yeye kumuingiza kazini Msaidizi wake, Mch. Michael Mlondakweli Kanju.
ILIVYOKUWA
Ibada ilianza kwa maandamano kutoka yalipo Makao Makuu ya Dayosisi hiyo, yaliyopo katikati ya Mji wa Lushoto na kuelekea Kanisa Kuu huku waki jipanga kwa kuongozwa na mbeba msalaba,

wabeba bendera ya Dayosisi na wapiga tarumbeta ambao walikuwa zaidi ya mia moja.Wapiga tarumbeta walikuwa kivutio kikubwa kwani walikuwa mahiri katika upigaji wao, pia walikuwa na sare ya pamoja ya mashati meupe na suruali nyeusi kwa wanaume na wanawake sketi nyeusi.

Nyuma ya kwaya ya tarumbeta kulifuatiwa na waimbaji wa kwaya mbalimbali kutoka ndani na nje ya Dayosisi, waumini na wageni, mwenzi wa Askofu Mteule na Msaidizi wa Askofu, kisha Wachungaji wa Kanisa hilo pamoja na wageni kutoka maeneo mbalimbali.Kwa ujumla kulikuwa na watu wengi katika maandamano hayo ambao yalikuwa yakiongozwa na Askari kutoka jeshi la olisi na Magereza ambao walitoa ushirikiano mzuri.

Maandamano yalipofika Kanisa Kuu yalipokelewa na Maaskofu, Wasaidizi wa Maaskofu, Wakuu wa Majimbo na Wachungaji.
KUANZA KWA IBADA
Ibada iliongozwa na Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mch Dkt. Alex Malasusa kwa upande wa Liturgia na mahubiri yalitolewa na Mkuu wa Kanisa la KKKT Dkt. Fredrick Shoo, ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini.
Baada ya hatua ya mahubiri Askofu Dkt. Malasusa alitangaza hatua ya pili ya Ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule Dkt. Msafiri Mbilu na hatua hiyo iliongozwa na Askofu Dkt. Solomon Massangwa wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Kati na Askofu Andrew Gulle wa KKKT-Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria (Mwanza).
Kabla ya hatua hiyo Katibu Mkuu Mteule wa Dayosisi hiyo, Mch. Godfrey Tahona Walalaze, alitoa tamko la kuridhiwa Mch. Dkt. Msafiri Mbilu kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa KKKT-DKMs na tamko hilo pia lilimtangaza Mwekaji wakfu Mkuu kuwa ni Askofu Dkt. Solomon Massangwa.
Askofu Dkt. Msafiri Mbilu alivalishwa pete ya uaskofu baadaye kuvalishwa vazi maalum la kiuaskofu kisha kofia na Maaskofu waliokuwa wakiongoza tukio hilo. Matukio yote hayo yalifanyika huku waumini wanashangilia kwa vifijo na nderemo.
Baada ya kuweka wakfu na kukabidhiwa kila kitu na kusaini hati ya uaskofu, Mkuu wa KKKT, Dkt. Shoo alimfuata Dkt. Mbilu na kumshika mkono kisha kumuingiza kazini rasmi kuwa Askofu wa KKKT-DKMs, pamoja na kumkalisha kwenye kiti maalumu cha uaskofu.
Tukio hilo lilitawaliwa na furaha kubwa na kisha Mkuu wa Kanisa alimsimamisha Askofu Mbilu na kumtaka ageukie washarika wake.
Askofu Dkt. Shoo: Dk. Mbilu usiogope, Mkuu wa KKKT, Dkt. Fredrick Shoo wakati wa mahubiri, alitolea mfano wa Mussa na Joshua na kumtaka Dkt. Mbilu aongoze Dayosisi kwa kumtegemea Mungu na siyo kwa akili yake.

Pia alimtahadharisha kuwa hata katika nafasi ya uaskofu bado atakutana na magumu ila asiogope wala kukata tamaa, maana aliyemuita ni Mkuu kuliko hayo atakayokutana nayo na kumweeleza kuwa amuite Mungu naye atamheshimisha.
Mkuu wa KKKT pia alimuomba Askofu Dkt. Mbilu ajue kuwa Dayosisi hiyo amewekwa na Mungu na siyo yake.

“Iwe yako kwa sababu miongoni mwa Wachungaji walio wengi umeteuliwa kuongoza, lakini siyo mali yako kwa kuwa unaweza kuiendesha utakavyo. Bali uwe tayari kutumika kama chombo kufuata na kusikiliza sauti ya Mungu, kwa kuwa Mungu ana muongozo usiokosea,” alisema Askofu Dkt. Shoo.
“Mumuombee Askofu na msaidizi wake na upendo mtakaouonesha kwao itakua chachu kutimiza kuwajibika na kutimiza yale ambayo Mungu amewaitia. Askofu Dkt. Shoo pia aliiambia Halmashauri ya Dayosisi kuwa inayo kazi ya kumshauri na kumuombea na kumkumbusha kwa hekima yale afanyayo.
UTANI WA MZEE MAKAMBA WAACHA UJUMBE MZITO
Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Mzee Yusuph Makamba ambaye alikuwa mmoja wa wageni walioalikwa katika Ibada hiyo wakati akitoa salamu zake alianza kwa utani, jambo ambalo lilifanya muda wote aliokuwa akizungumza watu walikuwa wakicheka.
Makamba alitoa wito kwa Askofu Dkt. Mbilu kuwa asiwe mbinafsi kwenye kuongoza bali atumie wasaidizi wake ili kazi ya Mungu isonge mbele zaidi.
“Askofu Mbilu una msaidizi wako anaitwa Kanju, pia una Wajumbe wa Halmashauri Kuu, Wachungaji, Wazee wa Kanisa, Wainjilisti na Mashemasi pamoja na watendakazi wengine hakikisha una watumia ili uweze kusogea na kazi ya Mungu ionekane.”
Awali Mzee Makamba alisema kuwa yeye ni muislamu lakini angebatizwa angekuwa Mlutheri kwa kuwa alisoma shule za misheni akiwa Darasa la tano mwaka 1955 na alifundishwa na Askofu Dkt. Sebastian Kolowa.
Alisema ukaribu wake na Askofu Kolowa uliimarika kwa yeye kupenda kula makande, ‘pure’ kwa lugha ya kisambaa.“Ikifika muda wa kula mke wa Askofu Kolowa ananiambia basi nami naenda kula kwake.”Alisema Askofu alipofariki, mama Kolowa alimwambia; ‘Mzee amefariki lakini bado Makamba hujabatizwa kwa nini?’Mzee Makamba alipokuwa akijiandaa kujibu Askofu Kweka ambaye alikuwa karibu naye akamuuliza unasubiri nini? Hata leo nipo tayari kukubatiza.
“Ndipo nikamwambia ‘ukinibatiza leo nipe leo Kanisa na unipangie Usharika wa Bumbuli,’ akakataa, toka siku hiyo hata leo sikubatizwa ila naomba mama Kolowa endeleeni kuniombea,” alisema.Mzee Makamba alimalizia pia kwa kutoa zawadi ya mabati 100 kwa Dayosisi hiyo ambayo, alimtaka Askofu Mbili achagua wapi pa kuyalekeza kwa kazi ya Mungu.Na ahadi hii aliitimiza. “Upendo ni kutoa, nami natoa mabati 100 ambayo wewe utajua uyaelekeze wapi kwa kazi ya Mungu,” alisema.
ASKOFU DKT. MBILU USKOFU NI WITO WA KITUME
Askofu Dkt. Mbilu mbali na kushukuru Serikali na viongozi wake akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, pia alimpongeza Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa kwa namna ya utayari wake wa kushirikiana na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.
Askofu Dkt. Mbilu wakati akihutubia Kanisa wakati wa Ibada hiyo alisema Kanisa ni mali ya Kristo Yesu ambaye amelinunua kwa damu yake ya thamani.Alisema ameipokea Dayosisi hiyo kwa neema ya Mungu, hivyo ataongoza kadiri Mungu atakavyomtumia kwa maana ndiye aliyemuita kuwahudumia wote kiroho, kimwili na kiakili.
“Tuombeane, tushauriane na tushirikiane kwa pamoja katika kuimarisha Dayosisi yetu na watu wake wamjue Mungu kupitia mafundisho sahihi ya neno la Mungu, na kuimarisha vituo vya watoa huduma pamoja na miradi mingine ya Dayosisi ili kuimarika kiuchumi, kimaendeleo na kazi ya Mungu isonge mbele.”
WAZIRI MKUU ATOA TUMAINI KKKT-DKMs
Waziri Mkuu Majaliwa mara baada ya salamu zake, pia hakusita kueleza furaha yake kwa Lushoto kuwa ni miongoni mwa Wilaya zinazoongoza kutunza mazingira na zenye misitu ya asili na kutoa wito kwa kila kiongozi atakayekuwa Lushoto au Tanga, kuhakikisha kuwa ulinzi wa miti asili na misitu unaimarishwa
“Naungana na wengine kukupongeza, Wanadayosisi wanaimani kubwa na wewe, simamia maono na malengo, imarisha umoja na wanajamii pamoja na washarika,” alisema.
“Mafanikio ya Dkt. Mbilu yataimarika pale ambapo atapata ushirikiano wa wote, ili maendeleo yaonekane kwa haraka. Nitoe wito kwenu mpeni ushirikiano ili mfanikiwe na Mungu atawabariki,” alisema.
Akizungumzia Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU), alisema kwa sasa tayari anatarajia kuwa kila kitu kitaenda sawa. Alisema ofisi yake itaharakisha kuyapitia maombi kwa haraka na kuondoa vikwazo visivyo muhimu ili chuo hicho kiendelee.
“Kama ni deni na ulisema utalipa tutakupa muda ulipe huku shughuli zinaendelea, na suala la kukosekana wahadhiri wenye sifa basi tunao wengi na wewe Mbilu ndio mkuu wa chuo na unatosha, endeleeni kuboresha na kujiimarisha, ili kibali kikitoka basi muwe pazuri, mimi na ofisi niliyopewa dhamana kuiongoza msihofu katika hili nitalibebea bango.”
Alisema serikali inatambua mchango mkubwa wa Kanisa kwa watu wake, kwani imekuwa ikitoa mahitaji muhimu na kuwaongoza kiroho jambo ambalo linaleta malezi bora kwa watu.
“Serikali inatambua nchi haiwezi kwenda bila ushirikiano, na tukiimarisha uhusiano wa taasisi za dini na watu binafsi katika kuleta maendeleo, na mfano ushirikiano wa serikali na Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwenye upande wa uendeshaji vituo vya afya ili kila Mtanzania apate huduma hiyo kwa ukaribu zaidi.
MKUU WA KANISA LA ANGILKANA TANZANIA
Askofu Dkt. Mahimbo Mndolwa alimpongeza Askofu Dkt. Mbilu na kumkumbusha wajibu aliopewa sio wa Kanisa la Kilutheri pekee, bali ni wa kutunza roho za watu zisipotee.
“Umepewa wajibu huo mimi ni Askofu wa Anglikana, ukiwa huku milimani unawajibu na Wakristo wote hata wa Anglikana, nasi hivyo hivyo tukiwa tambarare tunawajibu na wote waaminio na wasio amini ili utume wa Mungu ukamilike na watu wamjue yeye.”
Awali Askofu Mndolwa pia aliomba serikali kuangalia namna ya kufufua zao la chai kama ilivyo zao la katani.“Kwa sasa maeneo ya Amani, Mkinda, Milimani Bumbuli zao hilo tegemezi limesuswa na kupelekea wananchi kuwa na mwamko mdogo.
“Ombi langu tuimarishieni na kuliinua zao hili la chai kwani bado linahitajika na lina soko kubwa, kufanya hivyo kutasaidia kuinua uchumi wa watu wa Tanga na kuirudisha Tanga kwenye hadhi yake ya mazao hayo.”
WAZIRI MKUU AZUNGUMZWA KILA KONA LUSHOTO
Waziri Mkuu Majaliwa mbali na kuwa ni muumini wa Kiislamu alitimiza wajibu wake wa kiuongozi lakini pia alionyesha uchaji mkubwa. Baadhi ya Washarika walimpongeza kwa uvumilivu wake wa kukaa zaidi ya saa saba kufuatilia Ibada hiyo ndefu bila hata ya kuchoka na wengi walimpongeza kwa uchaji wake.

ASKOFU DKT. MBILU AMUINGIZA MCH KANJU KAZINI
Baada ya kupewa mamlaka kamili ya kuiongoza KKKT-DKMs, Askofu Dkt. Mbilu alitumia taratibu za Kanisa la KKKT kumuingiza kazini msaidizi wake, Mch. Michael Mlondakweli Kanju.
Askofu Dkt. Mbilu baada ya kuita Wasadizi wa Maaskofu kufika mbele kumzunguuka na kumvalisha vazi maalum na kisha kumwingiza kazini, alimtambulisha rasmi kwa Waumini kuwa ndiye Msaidizi wake.

“Naomba uwageukie waumini wakuone, kisha naomba familia yako ije nayo iambatana nawe twende kwa mgeni rasmi.“Waziri Mkuu huyu ndiye Dean Kanju wa Dayosisi yetu napenda kumtambulisha kwako.”. Alimtambulisha wa Waziri Mkuu kama yeye alivyo pelekwa na Mkuu wa Kanisa kutambulishwa kwa Waziri Mkuu huyo. Muda wote huo Washarika hao walikuwa wakiimba na kupiga makofi na tarumbeta zikipulizwa.
ASKOFU WA MOROGORO AOMBEA WENZI
Katika Ibada hiyo iliyokuwa na furaha na nderemo karibu muda wote, Askofu Jacob Mameo wa KKKT-Dayosisi ya Morogoro, aliongoza sehemu ya maombi kwa kuwaombea wenzi wa Askofu na Msaidizi wake.
Askofu Mameo alimuombea Bi. Mary Mbilu ambaye ni mke wa Askofu Dkt. Mbilu pamoja na Bi. Joyce Mlondakweli Kanju ambaye ni mke wa Dean Kanju.
ASKOFU DKT. MBILU APIGA ‘MGUDULO’ WA KISAMBAA (UMUKAYAA)
Askofu Dkt. Mbilu kabla ya kuhitimisha hutoba yake, alimwambia Waziri Mkuu kwa utayari wake wa kuwa pamoja na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ameamua kumpa zawadi.
“Waziri Mkuu hata mimi ni muimbaji mzuri na ninapiga tarumbeta, leo wacha nikupigie ‘mgudulo’ wimbo wa tarumbeta ambao inapulizwa wakati wa sherehe.”
Askofu Dkt. Mbili alipopiga tarumbeta hilo, watu wengi walifurahi hadi Waziri Mkuu alifurahi na kupiga makofi kuonesha furaha yake kama ishara ya kupokea zawadi hiyo.


