
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ametoa wito kwa wazazi na walezi kutuma vijana wao kujiunga na masomo katika Taasisi ya elimu ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) na kuongeza kuwa ni vema kutumia muda huu ambao Taasisi ya KOTETI inaendelea kufanya udahili kwa kutuma maombi yao ilikujiunga na Taasisi hiyo.

Askofu Dkt. Msafiri Mbilu ametoa wito huo leo tarehe 18/06/2023 kwenye Ibada ya Kipaimara iliyofanyika katika Jimbo la Kaskazini Usharika wa Mwangoi Mtaa wa Mlesa. Ibada hiyo ilikuwa na matukio mbalimbali ikiwemo Kubarikiwa kwa jumla ya vijana wapatao 48 huku watatu kati yao wakibatizwa, Kufunguliwa kwa nyumba ya mtumishi pamoja na kuwekwa wakfu kwa vyombo vya muziki.

Katika risala ya vijana hao waliobarikiwa wametoa shukrani zao za dhati kwa Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu kwa kufika na kuungana nao katika siku yao muhimu ya kuhitimisha mafundisho ya Kipaimara, kukiri Imani,kuombewa na kubarikiwa kwao.

Pamoja na vijana hao kukiri kufundishwa msingi wa Imani yao wameahidi kuungana na Baba Askofu Mbilu pamoja na kumuombea ili atimize maono ya kuiendeleza Dayosisi na kuleta maendeleo.

Taasisi ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) ipo Wilayani Lushoto Mkoani Tanga na inamilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, huku ikiwa na usajili wa NACTVET kwa Namba. KOTETI/HAS/249 na sasa inatangaza nafasi ya masomo kwa muhula mpya wa Masomo 2023/2024, kwa kozi ya PHARMACY YAANI ORDINARY DIPLOMA IN PHARMACEUTICAL SCIENCES – KWA MIAKA 3.



