
Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt. Msafiri Joseph Mbilu,ni mmoja wa wageni walioalikwa kwenye hafla ya Chakula cha Jioni iliyoandaliwa na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania . Hafla hii ilifanyikia tarehe 31/10/2023 katika ukumbi wa Sea Cliff Hotel Jijini Dar es Salaam ikiwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo wenye ushirikiano na Ujerumani.Hapa Baba Askofu Dkt. Mbilu alialikwa kwa mwaliko maalumu kutokana na uhusiano mkubwa uliopo na wa muda mrefu kati ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Ujerumani.

RAIS wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, anafanya ziara ya kikazi nchini Tanzania iliyoanza Oktoba 30 hadi 01 Novemba 2023.Ziara hiyo mbali na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kimaendeleo baina ya Tanzania na Ujerumani, pia imelenga kwenye kukuza na kuimarisha misingi ya biashara na uwekezaji.
“Ujumbe wa Rais Steinmeier utajumuisha viongozi wengine wa serikali, pamoja na wawekezaji wa makampuni makubwa 12; utawasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam, 30 Oktoba 2023 na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba,” imeeleza taarifa hiyo.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Akiwa nchini, Rais Steinmeier atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam, Oktoba 31, 2023. Baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao watapata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari kuelezea kuhusu masuala muhimu yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo yao.
Marais hao watapata fursa ya kushiriki katika Jukwaa la Biashara, litakalohusisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizo mbili, lililoandaliwa na Ubalozi wa Ujerumani kwa ushirikiano na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika Hoteli ya Hyatt Regency; ambapo pamoja na mambo mengine, viongozi hao watapokea taarifa iliyojadiliwa na Jukwaa hilo.
“Siku ya tarehe 01 Novemba 2023, Mheshimiwa Rais Steinmeier atasafiri kwenda wilayani Songea, mkoani Ruvuma kutembelea Makumbusho ya Vita vya Majimaji na Shule ya Msingi ya Majimaji.
Hii ni makumbusho pekee nchini Tanzania inayoonesha historia kubwa ya Vita vya Maji Maji katika harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Wajerumani,” imeeleza taarifa hiyo
Tanzania na Ujerumani zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliodumu kwa muda wa miaka zaidi ya 60.
Nchi hizi mbili zimekuwa zikishirikiana kwenye sekta mbalimbali za kimkakati hususan biashara na uwekezaji, maji, afya, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake, uhifadhi wa bioanuai, usimamizi wa fedha, utalii pamoja na malikale na utamaduni.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Tanzania imekuwa ikiuzia Ujerumani bidhaa zenye thamani ya wastani wa Dola za Marekani milioni 42.04 kwa mwaka. –
Bidhaa kuu ambazo Tanzania inaiuzia Ujerumani ni pamoja na kahawa, tumbaku, pamba, asali, samaki, nta na vito vya thamani.
Kadhalika, Tanzania inaagiza bidhaa kutoka Ujerumani zenye wastani wa Dola za Kimarekani milioni 237.43 kwa mwaka na bidhaa kuu zinazoagizwa kutoka Ujerumani ni Dawa, Vifaa Tiba, Mafuta (manukato, vipodozi) Magari, Vifaa na Mashine za Umeme.
Kwa upande wa uwekezaji, Ujerumani ni miongoni mwa nchi kumi zinazoongoza kwa uwekezaji nchini. Kwa mujibu wa TIC hadi kufikia Agosti 2023, miradi 178 ya Ujerumani yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 408.11 ilisajiliwa na kutoa fursa za ajira zipatazo 16,121.
Kwa upande wa Zanzibar, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imefanikiwa kusajili miradi 15 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 300.00 ambayo imezalisha ajira 905.
Kampuni za Kijerumani zilizowekeza nchini zinajihusisha zaidi na sekta za kilimo, viwanda, nishati mbadala, ujenzi, utalii sanaa na utamaduni. Kufanyika kwa ziara hii ni ushahidi tosha kuwa Diplomasia ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inazidi kupaa.

