Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa amesema kuwa ushiriki wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ibada Maalumu ya yeye kuingizwa kazini kuipngoza KKKT imeonyesha ni kwa namna gani Serikali yake inavyoshirikiana vizuri  na madhehebu yote ya dini na taasisi zake hapa nchini.

Askofu Dkt. Malasusa ameongeza kuwa uwepo wa Rais Samia ni mwendelezo wa Taifa kuonyesha ulimwengu namna gani Serikali na dini zinavoweza kushirikiana kwa upendo na amani katika mambo mbalimbali.Sambamba na hayo Mkuu wa KKKT Askofu Dkt. Malasusa ameahidi kuendeleza mambo mbalimbali ambayo yameanzishwa na mtangulizi wake Askofu Dkt Fredrick Shoo, ikiwemo suala la katiba moja ya Kanisa la KKKT.

 

Huyu ndiye Askofu Dkt Alex Gehaz Malasusa
Askofu Dkt. Alex Malasusa alizaliwa Aprili 18, 1961 katika kitongoji cha Kiwira, Kijiji cha Lukinga Wilaya ya Rungwe. Wazazi wake ni marehemu Mchg. Gehaz Japhet Malasusa na Subiliga Timothy Mwakimi. Alibatizwa na Mch Amon Mtwawa mwezi Julai 1961 katika Usharika wa Igonwe, Rungwe. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Rungwe (mwaka 1967-1969) na Bungo Morogoro mwaka (1970-1972). Alipata elimu ya sekondari kati ya mwaka 1973 hadi 1976 na alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Kigurunyembe kati ya mwaka 1978-1980. Mwaka 1981 - 1983 alijiunga na Chuo cha Biashara (College of Bussiness Education - CBE) jijini Dar es Salaam ambako alihitimu Stashahada ya Usimamizi wa Biashara (Diploma in Bussiness Administration).

Wakati huo pia alikuwa mtumishi wa uliokuwa Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi (National Provident Fund - NPF)akifanya kazi katika Idara ya Ukaguzi wa Hesabu. Kati ya 1988- 1995 alikuwa mwanafunzi katika Chuo cha Theolojia Makumira. Alianza akiwa mwanafunzi wa kozi ya cheti katika Theolojia lakini kabla ya kumaliza kozi hiyo, alifanya na kufaulu mitihani maalumu wa kujiunga na shahada ya kwanza katika Theolojia (Bachelor of Divinity - BD) mwaka 1995. Baada ya kuhitimu, alibarikiwa kuwa Mchungaji Septemba 3,1995 katika Usharika wa Maneromango. Aliyeongoza ibada ya kumbariki Dkt. Malasusa kuwa Mchungaji ni aliyekuwa Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani kwa wakati huo, Askofu Elinaza Sendoro.

Baada ya kubarikiwa Mchungaji Malasusa alipangwa kutumika sharika za Mburahati na baadaye Kisarawe. Akiwa Kisarawe alipewa pia wajibu wa kuongoza Seminari ya Kilutheri Kisarawe. Sharika nyingine alizotumikia ni Yombo na Msasani; na akiwa Msasani pia alikuwa Mkuu wa Jimbo la Kinondoni (wakati huo). Mwaka 1994- 1996 alisoma kwa njia ya posta katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na mwaka 1996 - 1997 alisoma kwa njia hiyohiyo katika Chuo cha Theolojia Vancouver, Canada akichukua mafunzo ya muda mfupi kuhusu malezi ya vijana.

Pia alichukua masomo ya mwaka mmoja (1999-2000) yanayohusu lugha ya Utamaduni wa Kifaransa kwenye chuo kilichoko mjini Paris. Desemba 21, 1996 Mch. Malasusa alifunga ndoa na Ericah Simon Nkonoki katika Usharika wa Azania Front. Mpaka sasa Askofu Malasusa na mkewe wamejaliwa watoto watatu; Miriam, Michael na Mercy. Mwaka 1994 -2004 Mch. Malasusa aliitwa katika Umoja wa Kimisioni wa Kiinjili (United Evangelical Mission - UEM), nchini Ujerumani na baada ya kufaulu kwenye usaili alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya vijana barani Afrika. Wakati akiendelea na wajibu huo, alichaguliwa kuwa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP). Nafasi ya Uaskofu wa DMP, ilimpa fursa ya kuchaguliwa kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjli la Kilutheri Tanzania (KKKT), katika uchaguzi uliofanyika Julai 18, 2017 katika Chuo Kikuu cha Makumira, Arusha.


Katika umri wake mdogo kuliko maaskofu wote waliomtangulia kushika nafasi ya Mkuu wa Kanisa, Askofu Dkt. Malasusa alipokea wajibu wa kuliongoza KKKT kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Kanisa wa wakati huo, Hayati Askofu Dkt. Samson Mushemba na kuingizwa kazini rasmi akiwa Mkuu wa nne wa KKKT Novemba 11, 2007, kwenye Ibada iliyofanyika katika Usharika wa Azania Front, Dar es Salaam. Baada ya kutumika katika kipindi kilichotajwa kwenye Katiba ya KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Askofu Dkt. Malasusa alipigiwa kura kwa mara ya pili kwenye Mkutano Mkuu wa 29 uliofanyika Bagamoyo Novemba 29,2010 na kuchaguliwa tena baada ya kupata kura ambazo zilimpa ushindi hivyo kuwa Askofu wa kudumu ambaye hataoondolewa tena uongozini kwa njia ya kura hadi atakapostaafu. Wakati akiendelea na kuiongoza Dayosoi ya Mashariki na Pwani (DMP), Askofu Dkt. Malasusa aliweka rekodi mpya kwa kuchaguliwa awamu nyingine kuwa Mkuu wa KKKT katika Mkutano Mkuu wa Kanisa wa 21, uliofanyika Agosti 2023, Chuo Kikukuu cha Tumaini Makumira, Mkoani Arusha na atakaa katika nafasi hiyo hadi pale utakapofanyika uchaguzi mwingine miaka minne ijayo. Ask. Dkt. Malasusa anaongoza Kanisa hilo kwa mara ya pili, kwani aliwahi kuongoza mwaka 2007-2015, alipokabidhi kwa Ask. Dkt. Fredreick Shoo.


Katika utumishi wake, Askofu Malasusa ameshika nyadhifa nyingine kadhaa, ndani na nje ya Tanzania ambazo ni pamoja na kuwa Mwenyekiti wa mradi wa Mahusiano kati ya Wakristo na Waislamu barani Afrika, Makamu wa Pili wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania - CCT (kuanzia mwaka 2010), Makamu wa Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani barani Afrika (Kuanzia 2010) na Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Viziwi Tanzania (Kuanzia2010). Kwa kutambua utumishi wake uliotukuka, Askofu Dkt. Malasusa ametunukiwa shahada tatu za Uzamivu kutoka Chuo cha Kilutheri cha Utatu Mtakatifu kilichoko Amerika (Novemba 8, 2009), Chuo Kikuu cha Finlandia kilichoko Hancock Michigan America (Mei 2, 2010) na Chuo Kikuu cha Helsink (Mei 28, 2011).